VIGOGO CHUONI ARUSHA ( IAA) WAFIKISHWA KIZIMBANI


Wafanyakazi 11 wa Chuo Cha Uhasibu Arusha, wakiwa katika Makahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha jana,  walikofikishwa na kusomewa mashtaka manne ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 6.2 milioni. Picha na Peter Saramba
KWA UFUPI
  • Katika shtaka la kwanza, Profesa Monyo na mwenzake Jerome Augustine ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ununuzi chuoni hapo wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuhamisha umiliki wa Solar Power Back-up Kit yenye thamani ya Sh6.2 milioni, mali ya chuo na kuifanya mali binafsi ya mkuu huyo wa chuo.

Arusha.  Vigogo 11 akiwamo Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (AA), Profesa Johannes Monyo, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kosa la uhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali.
Katika shtaka la kwanza, Profesa Monyo na mwenzake Jerome Augustine ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ununuzi chuoni hapo wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuhamisha umiliki wa Solar Power Back-up Kit yenye thamani ya Sh6.2 milioni, mali ya chuo na kuifanya mali binafsi ya mkuu huyo wa chuo.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Kilongozi Adama aliyekuwa akisaidiana na Wakili Hamidu Simbano alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Mustapha Sayani kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Septemba 30, 2011 kinyume cha kifungu cha 31 cha sheria namba 11 ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007.
Shtaka la pili linawakabili wajumbe wa bodi ya zabuni wa chuo hicho, Jerome Augustine, Chacha Wambura, Mpoki Mwasaga, Papias Njaala, Mathew Melita, Mary Thomas, Elisaria Kisanga na Gerald Malisa ambao kwa pamoja wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kuruhusu ununuzi wa kifaa hicho cha Umeme Jua kinyume cha sheria.
Katika shtaka la tatu, Wakili Adam alidai kuwa kati ya Novemba Mosi na 30, mwaka 2011, washtakiwa Jerome Augustine, Faraji Mnyepe na Honory Mkelemi walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaidia malipo ya Sh6.2 milioni kwa ajili ya kifaa hicho cha umeme jua kinyume cha sheria.
Shtaka la nne linawakabili washtakiwa Johannes Monyo na Jerome Augustine wanaodaiwa kuwa mnamo Julai 26 na Novemba 30, mwaka 2011, kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa Chuo cha uhasibu, waliisababishia taasisi hiyo hasara ya Sh. 6.2 milioni kinyuma cha kifungu cha 31 ya sheria namba 11 ya makosa ya kupambana na kuzuia rushwa ya mwaka 2007.
Kabla ya kuwasomea watuhumiwa mashtaka yao, Wakili Adam aliiomba Mahakama kutoa hati ya kuwakamata washtakiwa namba tano Mpoki Mwasaga, namba Saba Mathew Melita na namba 10 Gerald Mkelemi ambao hawakuwepo mahakamani jana, ombi lililokubaliwa kwa Hakimi Siyani kutoa hati hiyo.
Upande wa mashtaka pia uliomba kubadilisha jina la mshtakiwa wa nne Chacha Wambura ambaye awali jina lake liliandikwa Chacha Makamba Augustine, Mahakama ilikubali ombi hilo.
Upelelezi wa shauri hilo lililovutia umati mkubwa wa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo cha Uhasibu umekamilika na itatajwa Agosti Mosi, mwaka huu ambapo washtakiwa watasomewa maelezo ya awali ya kosa.
Awali kabla ya Mahakama kuanza, kulitokea mvutano kati ya kundi la waandishi wa habari, ndugu, jamaa, marafiki na wapambe wa watuhumiwa waliokuwa wakijaribu kuzuia upigaji wa picha kabla ya hakimu kuingia.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA

HILI NDILO BIFU KUBWA KATI YA RIHANA NA NICK MINAJ.