JESHI LA POLISI LAOMBA MSAADA KUTOKA JESHI LA JWTZ KUSAIDIA VITA DHIDI YA MAJAMBAZI

Siku moja baada ya majambazi kuvamia Benki ya Access Tawi la Mbagala Rangi Tatu, kuua watu watatu akiwamo Polisi na kujeruhi watu wengine watatu akiwamo polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema wataomba msaada wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ili kukabiliana na matukio ya ujambazi.

Alisema Jeshi la Polisi linajipanga upya kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani kwa kuwashughulikia majambazi popote walipo.

Waziri Kitwanga alisema wanaanza na Mkoa wa Pwani, kwa kuhakikisha wanawasaka na kufyeka mapori yote ya Bagamoyo na kwingineko ili kuvunja mtandao wao.



“Kama walidhani Jeshi la Polisi limelala lipo macho, walichofanya ni kama wamemuamsha aliyelala, tutawasaka, tutawakamata na tutawapeleka kwenye mkono wa sheria na tutahakikisha tunawamaliza wote,” alisema Kitwanga.


Alisisitiza kuwa wanaotumia pikipiki nguvu ya ukaguzi itaongezwa dhidi ya vyombo hivyo, kwa sababu inaonekana wahalifu wengi hasa majambazi hutumia usafiri huo kutekeleza uovu wao.



Akielezea tukio la uporaji wa Mbagala, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wamefanikiwa kuwaua majambazi watatu kati ya 12 waliofanya uvamizi huo.


Alisema majambazi hao walikufa baada ya kupigwa risasi katika majibizano ya risasi na Polisi katika Kijiji cha Chui Mkuranga, baada ya kujaribu kutoroka walipozidiwa nguvu.



Alisema majambazi hao wakiwa na pikipiki sita, huku kila moja ikiwa na majambazi wawili waliokuwa na bunduki aina ya SMG na mabomu ya kutupa kwa mkono, walivamia benki hiyo na kuwashambulia kwa risasi kisha kuwajeruhi wafanyakazi wa benki hiyo waliokuwa katika chumba cha kuhifadhia fedha.



Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Salum Juma na Francis Amani, na kupora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa kati ya Sh20 na 30 milioni za kaunta baada ya kushindwa kuvunja chumba cha kuhifadhia fedha.



Alisema kabla ya kuingia ndani, walivamia kibanda cha walinzi na kumpiga risasi askari mwenye namba H7739PC Khalid Juma ambaye alifariki dunia papo hapo.



Pia, walimjeruhi kwa kumpiga risasi kwenye nyonga askari Shaban, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili na kupora bunduki mbili.



Kamanda Sirro alisema majambazi hao baada ya kufanya uporaji walipokuwa wanaondoka, walifyatua tena risasi iliyompata kidevuni na kumuua papo hapo Abdi Salum, ambaye ni muuza duka jirani na benki hiyo na Baraka Fredrick, mlinzi wa kampuni ya Security Group of Africa.



“Hata hivyo Polisi wamefanikiwa kukamata bunduki tatu kati ya hizo mbili ni mali ya Polisi, mabomu matatu ya kutupa kwa mkono na pikipiki sita zilizokuwa zikitumiwa na majambazi hao walipozidiwa nguvu walizitelekeza na kukimbia,” alisema Sirro.



Katika hatua nyingine, Februari 18, eneo la Kiwalani polisi walikamata majambazi watatu wakiwa na bastola moja na Februari 24 eneo la Upanga karibu na Daraja la Sarender, askari waliwakamata watuhumiwa watatu kwa makosa ya kujihusisha na ujambazi wa kutumia silaha.





Kamanda Sirro alisema baada ya kuwahoji walikiri kufanya matukio ya ujambazi wa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam.




“Alipofuatwa nyumbani kwake, alikutwa na sare za jeshi hilo, redio ya upepo na pingu,” alidai kamanda huyo

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA

HILI NDILO BIFU KUBWA KATI YA RIHANA NA NICK MINAJ.