HII NDIYO TOFAUTI KATI YA RAIS MAGUFULI NA RAIS MSTAAFU KIKWETE NDANI YA SIKU 100




Wakati Kikwete aliyeapishwa Desemba 21, 2005 alitumia siku tano kati ya 100 kuwaanda watendaji wake kufanya semina elekezi katika Hoteli ya kifahari ya Ngurdoto, Arusha ili kuwajengea uwezo mawaziri na makatibu wakuu, Dk Magufuli alisema mawaziri wake wasingepata semina hiyo, bali wangejifunza humo humo kazini na aliokoa Sh2 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa kazi hiyo.
Dar es Salaam. Kasi ya utendaji wa Rais John Magufuli ndani ya siku 100 akiwa ofisini imeendelea kujidhihirisha kuwa ni tofauti na ya mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.
Dk Magufuli ameibainisha wazi sura yake ya kubana matumizi na kuongeza mapato ya Serikali kwa kuzuia safari zisizo za lazima kwenda nje ya nchi, wakati katika utawala wa Kikwete safari zilikuwa nyingi na ndiyo maana  mmoja ya mawaziri wake alisema “tulikuwa tukigongana angani utadhani chini kuna moto.”
Wakati Kikwete aliyeapishwa Desemba 21, 2005 alitumia siku tano kati ya 100 kuwaanda watendaji wake kufanya semina elekezi katika Hoteli ya kifahari ya Ngurdoto, Arusha ili kuwajengea uwezo mawaziri na makatibu wakuu, Dk Magufuli alisema mawaziri wake wasingepata semina hiyo, bali wangejifunza humo humo kazini na aliokoa Sh2 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa kazi hiyo.
Hata makatibu wakuu waliofanyiwa semina, ilikuwa ya siku moja katika ukumbi wa Ikulu na pengine Kikwete aliona fedha nyingi zilizokuwa zinapotea katika kumbi za hotelini, akaamua kujenga ukumbi huo wa Ikulu.
Tayari Serikali ya Magufuli imekwishatangaza kuwa itakuwa inatumia ukumbi huo na kumbi nyingine za Serikali kufanyia mikutano na semina mbalimbali ili kupunguza matumizi.
Baada ya semina elekezi iliyowahusisha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, Kikwete aliendelea pia kutembelea kila wizara na kuwataka mawaziri wake kuandaa mipango ya kazi katika wizara zao, tofauti na Magufuli aliyetembelea wizara moja tu ya Fedha na kuhimiza uchapaji kazi, ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi.
Rais Magufuli katika kipindi hicho alikuja na mpango wake wa kubana matumizi ili fedha zitakazookolewa zitumike katika kutoa huduma kwa wananchi na hasa katika sekta za elimu na afya.
“Hakutakuwa na semina elekezi, hata sisi tulipoapishwa tulianza kazi mara moja. Waziri Mkuu alijielekeza bandarini kwenye makontena, Makamu wa Rais alijielekeza kwenye usafi wa mazingira. Mawaziri watajifunza wenyewe humohumo wizarani,” alisema Rais Magufuli wakati anatangaza Baraza la Mawaziri.
Makusanyo ya mapato
Wakati Kikwete anaingia madarakani makusanyo ya mapato yalipungua ndani ya siku 100 za utawala wake. Kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu, mapato ya  Desemba 2005 yalikuwa Sh190 bilioni na kupungua mpaka kufikia Sh157 bilioni Februari, 2006 kinyume na hali ilivyo wakati wa Dk Magufuli.
Mapato ya Serikali ya JK yalipungua kwa sababu ya mgawo wa umeme uliokuwa unalikabili Taifa baada ya kuchaguliwa kwake. Viwanda vingi vilisimamisha uzalishaji na vingine kufunga kabisa biashara zao, wakati Rais Magufuli alihimiza ukusanyaji kodi na kuwabana wakwepa kodi na kukusanya fedha zaidi ambazo zilikuwa zinapotea au zilizokuwa mikononi mwa wafanyabiashara wakishirikiana na watendaji wasiokuwa waaminifu.
Kutokana na hali hiyo, ndani ya siku 100 za Rais Magufuli, mapato ya Serikali yameongezeka. Mapato ya Desemba, 2015 yaliongezeka kutoka wastani wa Sh900 bilioni zilizokuwa zikikusanywa kwa miezi sita ya mwisho ya Kikwete mpaka kufikia Sh1.4 trilioni kwa mwezi.
Ongezeko hilo mbali na kodi, limetokana na jitihada za Rais Magufuli kubana matumizi yasiyo ya lazima zikiwamo safari za nje, mikutano, semina na kufuta sherehe za Uhuru zilizookoa Sh4 bilioni zilizotumika kwenye upanuzi wa barabara ya Morocco na Mwenge jijini Dar es Salaam.
Ziara za nje
Vilevile, katika kipindi hicho Rais Magufuli hajafanya ziara hata moja nje ya nchi, tofauti na Kikwete ambaye kabla ya Machi 31, 2006 alifanya ziara kadhaa katika nchi mbalimbali zikiwamo za kujitambulisha.
Miongoni mwa ziara hizo ni ile ya Januari 19-25 ya Khartoum, Sudan kuhudhuria mkutano wa nchi za Afrika (AU) , Machi  23 kwa ziara ya siku moja kujitambulisha Kigali, Rwanda,  Machi 22 Kampala, Uganda kwa ziara ya siku moja ya kujitambulisha na  Machi 24, Nairobi, Kenya.
Changamoto kuu
Siku 100 za Rais Kikwete zilikabiliwa na changamoto za ukame uliosababisha njaa katika maeneo mbalimbali ya nchi na ujambazi, ukiwamo uvamizi wa benki.
Vilevile katika kipindi hicho matukio mengi ya ujambazi yaliripotiwa sehemu mbalimbali za nchi na kutishia usalama wa wananchi na Kikwete alichukua hatua kwa kuanzisha wizara ya usalama wa raia ili kusimamia kwa karibu zaidi usalama wa wananchi.
Rais Magufuli amekuta changamoto za ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya ofisi. Mara baada ya kuapishwa, alianza kukabiliana na wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa kuwataka kulipa kodi zao.
Kiongozi huyo amewafukuza kazi watendaji mbalimbali wa Serikali waliobainika kutumia ofisi zao vibaya na kulisababishia Taifa hasara. Mpaka sasa, Rais Magufuli ametimua watendaji zaidi ya 150 wa Serikali na taasisi kwa makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.
Dk Magufuli amenukuliwa akisema ataendelea kufukuza wafanyakazi wazembe kwa mtindo wake maarufu wa ‘kutumbua majipu’. Anachotaka katika utawala wake ni uwajibikaji na uongozi unaojali watu wa chini.
Uteuzi wa mawaziri
Kikwete alikaa siku 14 baada ya kuapishwa (Desemba 21, 2005) bila kutangaza baraza lake la mawaziri kazi aliyoifanya Januari 4, 2006, alipoteua mawaziri na naibu mawaziri 60.
Kwa upande wa Rais Magufuli, alikaa siku 35 tangu alipoapishwa (Novemba 5, 2015) bila kutangaza baraza lake, mpaka Desemba 10, 2015 alipotangaza baraza lenye mawaziri na manaibu waziri 35 na kufanya baraza lake kuwa dogo ukilinganisha na lililopita.
Tofauti nyingine baina ya marais hao, ni kuwa wakati Rais Magufuli amepunguza mawaziri 21 kutoka 55 wa mwisho wa mtangulizi wake, Kikwete aliongeza 23 kutoka 37 wa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa.
Tofauti nyingine ya marais hao ni kuwa Kikwete aliingia madarakani na kauli ya ‘kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya’ wakati Magufuli amekuwa akitamba na ‘Hapa Kazi Tu’.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA

HILI NDILO BIFU KUBWA KATI YA RIHANA NA NICK MINAJ.