Zitto Kabwe kupewa Ulinzi Mkali
CHAMA cha Alliance Transparency For Change (ACT) Mkoa wa Kigoma, kimeahidi kumlinda na kumtetea Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), kutokana na changamoto zinazomkumba kupitia watu wachache wanaotaka kumwangusha kisiasa.
Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya chama hicho, Bw. Jaffar Kasisiko, aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Cine Atlas, kwenye Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Alisema chama hicho hakipo tayari kuyafumbia macho matatizo yanayomkuta Bw. Kabwe na kumshauri mbunge huyo aachane na CHADEMA badala yake ajiunge na ACT ili aweze kukusanya wanachama kuanzia ngazi ya kitongoji, vijiji, kata na wilaya.
Aliongeza kuwa, uongozi wa CHADEMA una hila ya kusambaza maneno kwa umma dhidi ya Bw. Kabwe ili kulinda masilahi yao binafsi badala ya kutetea haki za wanyonge.
“Kabwe asipoteze muda wa kulumbana na uongozi wa CHADEMA, huu ni wakati mwafaka kwake kufanya uamuzi makini wa kwenda kuifuta kesi dhidi ya chama chake mahakamani na kujiunga na ACT,” alisema Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Msafiri Wamalwa.
Katibu Mwenezi Wilaya ya Kigoma kutoka chama hicho, Anzoluni Kibela, alisema ACT imeandaa kadi kwa ajili ya Bw. Kabwe ambapo kuna wabunge 18 wapo tayari kujiunga na chama hicho kwenye uzinduzi rasmi ulipangwa kufanyika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Shaban Mambo, aliwasihi wananchi wamuunge mkono Bw. Kabwe atakapojiunga na chama hicho ili aboreshe hali ya usafiri wa reli ya kati kwa kuwaletea treni inayotumia umeme kwa gharama zake.
Baadhi ya wanachama wapya wa ACT akiwemo aliyekuwa Mweka Hazina wa CHADEMA Kigoma Ujiji, Bw. Hamidu Hamis na Katibu wa ACT wilayani humo, Bw. Haji Idd, walisema wamejiunga na chama hicho ili kuleta uwazi na uwajibikaji
Tupe maoni yako hapo Chini..
Maoni
Chapisha Maoni