Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia
Ujerumani imenyakuwa Kombe la Dunia kwa mara ya nne na kuwa timu ya kwanza ya Ulaya kulitwaa kombe hilo katika ardhi ya Amerika Kusini baada ya kuishinda Argentina goli moja kwa sifuri katika fainali
Washangiliaji waliomimika kwa maelfu kuangalia mechi hiyo ya aina yake walikuwa wakiishangiria Argentina, huku zaidi ya raia 100,000 wa Argentina wakiripotiwa kumiminika nchini Brazil kupitia mpakani na baharini, lakini hilo halikuwadumaza Wajerumani.
Mario Götze ndiye aliyeweka kimiani goli la kwanza na la pekee katika dakika 113 na hivyo kuiandika nchi yake kwenye kitabu cha historia ya ushindi wa Kombe la Dunia. Kwa mara ya kwanza Ujerumani ilishinda Kombe hilo mwaka 1954, kisha 1974 na 1990, wakati huo bado ikiwa imegawika kati ya mashariki na magharibi. Ushindi wa mara hii ni wa kwanza tangu mashariki na magharibi kurudi tena kuwa taifa moja la Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.
Huo ni ubingwa wa soka wa kwanza wa dunia kunyakuliwa na Ujerumani tokea kuungana upya kwa furaha kwa Ujerumani mbili ya magharibi na mashariki hapo mwaka 1990 na kuja wakati taifa likiadhimisha robo karne tokea kuanguka kwa Ukuta wa Berlin.
Wakiwa bado na marui rui ya ushindi wao mkubwa wa kichapo cha mabao 7-1 dhidi ya Brazil katika pambano la nusu fainali Jumanne iliopita, mamilioni ya Wajerumani walimiminika mitaani kuishangilia timu yao ya taifa ambapo mashabiki 200,000 wakusanyika nyuma ya Lango la Bradenburg mjini Berlin kuliangalia pambano hilo huku wengine mamilioni wakiliangalia kwenye bustani na vilabu vya pombe,vilabu vya michezo na sebule za nyumba nchini kote Ujerumani.
Idadi iliovunja rekodi ya watazamaji wa televisheni milioni 32.6 waliangalia pambano la Ujerumani na Brazil na idadi kubwa ya zaidi hiyo inatazamiwa kuliangalia pambano la Jumapili (13.07.2014) katika uwanja mashuhuri wa Maracana ulioko Rio Di Janeiro nchini Brazil.
Miongoni mwa waliomininika katika uwanja wa Maracana kuishangilia timu hiyo ya Ujerumani ni pamoja na Kansela Angela Merkel ambaye amekwenda Brazil akiandamana na Rais Joachim Gauck na wanasiasa kadhaa waandamizi ili kuiongezea ari timu hiyo chini ya kocha Joachim Loew.
Maoni
Chapisha Maoni