Coutinho amfunika Jaja
KWA UFUPI
Jaja amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga hadi 2016
Dar es Salaam. Kiungo mpya wa Yanga, Mbrazil Andrey Coutinho amemfunika mwenzake Genilson Santos ‘Jaja’ kwa umahiri wa kupachika mabao katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar es Salaam.
Uhodari wa Coutinho wa kucheka na nyavu ulithibitika kwenye mazoezi yaliyofanyika jana kwenye uwanja huo pale alipofanikiwa kumtungua kipa wa timu hiyo, Juma Kaseja mabao manne kati ya mashuti yake matano aliyopiga.
Coutinho anayemudu kutumia vizuri mguu wa kushoto alikuwa akimchambua kiurahisi Kaseja ambaye alifanikiwa kudaka shuti moja tu la Mbrazili huyo ambalo alipiga kwa mguu wake wa kulia.
Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa Jaja ambaye kati ya mashuti matano aliyopiga, manne yalidakwa na Kaseja na moja tu alitikisa wavuni.
Mbali ya Coutinho mchezaji mwingine wa timu hiyo aliyeonyesha makali katika kutikisa nyavu ni mshambuliaji Said Bahanuzi ambaye mashuti yake manne kati ya sita yalizaa mabao.
Pia, mambo yalionekana kuwa magumu zaidi kwa Jaja kwenye zoezi la kukimbia kuzunguka uwanja ambapo mchezaji huyo mwenye mwili mkubwa alishika mkia.
Wakati huohuo, Jaja jana alisaini rasmi mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga hadi 2016.
Kabla ya kusaini mkataba huo, Jaja alikuwa anasubiri tathmini ya kocha wa timu hiyo Marcio Maximo na msaidizi wake Leonado Neiva wote ni Wabrazili.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema usajili wa Jaja unakuwa ni wa pili msimu huu kwa wachezaji wa kimataifa baada ya awali kumsajili kiungo mshambuliaji Coutinho.
“Kazi yetu uongozi ni kutekeleza maelekezo ya kocha mkuu pamoja na benchi la ufundi, walitoa mapendekezo ya usajili kabla hawajaanza kazi na mengine baada kuwasili yote tunajitahidi kuyatekeleza ili kila kitu kiende safi,” alisema Beno.
Maoni
Chapisha Maoni