Diamond azua vurugu nyingine Uingereza

Mwanamuziki Diamond Platnumz.PICHA|MAKTABA 

KWA UFUPI
Alisema waliamuru watu warudishiwe fedha zao, hivyo walipanga mstari na kurudishiwa fedha zao, kila mmoja akiamuriwa kuondoka eneo hilo huku wenye klabu hiyo wakinyang’anywa leseni.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond Platnumz kwa mara nyingine tena usiku wa kuamkia jana alisababisha vurugu kubwa nchini Uingereza baada ya kushindwa kutumbuiza katika ukumbi wa LaFace Club uliopo jijini London.
Hii ni mara ya pili kwa Diamond kusababisha vurugu nchi za ughaibuni baada ya Septemba 1, kusababisha vurugu katika mji wa Stuttgart nchini Ujerumani aliposhindwa kufika kwa wakati ukumbini.
Akizungumza na gazeti hili, shuhuda wa tukio ambaye ni Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Uingereza, Flora Lyimo alionyesha wazi kukerwa na tukio hilo ambalo alieleza kuwa huenda likaharibu sifa ya nyota huyo ughaibuni.
Lyimo ambaye alihudhuria shoo hiyo alisema Diamond alisubiriwa na zaidi ya watu 200 tangu saa sita usiku bila nyota huyo kutokea na ilipofika saa 10:00 alfajiri, ndipo walipoanzisha vurugu kudai kurudishiwa pesa zao.
Shoo hiyo ambayo ilitozwa kiingilio cha pauni 20 sawa na fedha za Tanzania Sh54,280 iliishia kwa dosari ya aina yake baada ya polisi kulazimika kuingilia kati kusimamia urudishwaji wa fedha hizo.
Alisema waliamuru watu warudishiwe fedha zao, hivyo walipanga mstari na kurudishiwa fedha zao, kila mmoja akiamuriwa kuondoka eneo hilo huku wenye klabu hiyo wakinyang’anywa leseni.
“Ni jambo la ajabu na aibu kwa msanii ambaye Watanzania tunamtegemea atuwakilishe nje ya nchi anakubali vipi kutangazwa kwenye shoo kama hajalipwa pesa zake, watu wanamchukulia kama tapeli kwani yeye mwenyewe amewatangazia mashabiki wake halafu hajatokea.
“Wengi tunapata shaka kama hajashirikiana na huyo promota kwani hata huo ukumbi ambao shoo ilitakiwa kufanyika hauna jukwaa maalumu ambalo msanii anaweza kutumbuiza binafsi nilishangaa haikuwa eneo sahihi, lakini nikasema ngoja niende kumuunga mkono Mtanzania mwenzangu,”alisema Lyimo.
Hata hivyo, pesa zilizopatikana hazikutosha kuwarudishia watu wote ikizingatiwa kuwa wengi walikata tiketi kabla ya siku ya shoo, hapo ndipo vurugu zilipotokea na polisi kulazimika kumshikilia promota wa shoo hiyo ambaye alifahamika kwa jina la Victor.
“Polisi wengi sana waliofika hapa ukumbini kwa ajili ya kulinda usalama, walichokifanya ni kumchukua promota aliyeandaa shoo hii na kumweka chini ya ulinzi kwa kosa la utapeli, kwa sharti kwamba mpaka watakapompata Diamond, lakini mpaka sasa bado haijajulikana alipo,” alisema Lyimo.
Lyimo alionyesha wasiwasi wake na kueleza kuwa kutokana na mfululizo wa matukio hayo huenda Diamond akazuiliwa kufanya shoo katika nchi za Ulaya, kutokana na kuanza kupoteza imani kwa mashabiki wake.
Gazeti hili lilimtafuta balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe ambaye alieleza kwamba hafahamu chochote kuhusu tukio hilo na kuahidi kulifuatilia kujua undani wake.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA

HILI NDILO BIFU KUBWA KATI YA RIHANA NA NICK MINAJ.