Ni mzobemzobe bungeni

Makachero na askari wa Kikosi cha Kutuliza
Makachero na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge baada ya kuitwa na Mwenyekiti Andrew Chenge ili kuwatoa kwa nguvu wabunge wa upinzani kwa kukaidi amri ya kuwataka waende nje jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
By Fidelis Butahe, Mwananchi
Dodoma. Polisi 35 jana walitumika kuwatoa ukumbini wabunge kutoka vyama vya upinzani baada ya vurugu kutokea ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na tangazo la uamuzi wa Shirika la Utangazaji (TBC) kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge.
Wabunge wa upinzani walitolewa ukumbini wakiwa wamebebwa juu juu au mzobemzobe, wengine wakiwa wamechaniwa nguo na wengine kurushiana makonde na polisi katika tukio lililoweka taswira ya kwanza ya aina yake tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992.
Waandishi wa habari waliokuwa ndani ya ukumbi wa Bunge, walizuiwa kwanza kuchukua picha za matukio yaliyokuwa yakiendelea ukumbini hapo, na baadaye kuondolewa na kupelekwa kwenye chumba kingine na hivyo kushindwa kufanya vizuri kazi yao ya kuchukua habari.
Kabla ya purukushani hizo kuanza, asubuhi kituo cha televisheni cha TBC1 kilikatisha matangazo yake ya moja kwa moja mara baada ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye kutangaza uamuzi wa chombo hicho kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge. Baadaye kituo cha televisheni cha Star TV nacho kikakatisha matangazo na hivyo kubakia Azam TV tu.
Lakini jioni, wakati mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akijiandaa kutangaza uamuzi wa kuwaondoa ukumbini wabunge wa Ukawa, mtangazaji wa Azam TV naye akatangaza kuwa kituo hicho kinakatisha matangazo hayo ya moja kwa moja.
Dalili za vurugu hizo zilianza kuonekana asubuhi wakati wabunge wa upinzani walipopinga kujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa Novemba 20 wakati TBC ikiwa imezima matangazo ya moja kwa moja, wakidai wananchi wana haki ya kusikia kinachojadiliwa.
Hoja hiyo ilisababisha Chenge kuahirisha shughuli za Bunge kuipa nafasi Kamati ya Uongozi kujadili na kutolea uamuzi hoja ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ya kupinga mjadala wa hotuba ya Rais kutorushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa.
Chenge aliahirisha shughuli hizo hadi saa 10:00 jioni wakati vurugu zilipoibuka.
Baada ya mvutano wa dakika 35 kati ya Chenge na wabunge wa upinzani kuhusu kanuni, vurugu hizo zililipuka saa 10:50 jioni.
Askari hao walitumia takriban dakika 25 kuwatoa wabunge hao ukumbini baada ya kuanza mzobemzobe huo saa 10:50 jioni na kuumaliza saa 11:15 jioni.
Wabunge hao walizua sintofahamu baada ya Chenge kueleza uamuzi wa Kamati ya Uongozi iliyokutana jana mchana kujadili hoja iliyotolewa asubuhi na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo, Kigoma Mjini), kupinga kusitishwa kurushwa kwa matangazo hayo, kauli ambayo ilisababisha mwenyekiti huyo kuahirisha kikao hicho mpaka saa 10:00 jioni kutokana na shinikizo la wabunge wa upinzani.
Wakati wabunge wakibebwa juu juu na askari hao, ofisa habari wa Bunge, Owen Mwandumbya aliwataka waandishi wote wa habari kutofanya chochote, ikiwa pamoja na kupiga picha, na kuwataka watoke nje ya ukumbi wa Bunge hadi kwenye eneo maalumu lililokuwa na ulinzi wa askari.
Akieleza uamuzi wa kamati ya uongozi, Chenge alisema: “Kwanza kamati imesema mwenyekiti wa Bunge alikuwa sahihi kuahirisha Bunge, pili hakuna haki iliyovunjwa, tatu kamati imeagiza mjadala wa hotuba ya rais uendelee na nne endapo kuna mbunge hajaridhika ni haki yake  kutumia kanuni ya 5 (4) ya kanuni za Bunge ili kuwasilisha malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge”.
Uamuzi huo uliwanyanyua wabunge wa upinzani. Safari hii mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliomba mwongozo wa suala hilo, akisema kuwa lilipaswa kutolewa uamuzi na mwenyekiti wa Bunge au Spika na  si kamati ya uongozi.
Katika hoja yake ya pili, Lissu alisema suala hilo ni la kikanuni na lilipaswa kutolewa ufafanuzi na Kamati ya Kanuni na si Kamati ya Uongozi, jambo ambalo lilipingwa na Chenge aliyesema kuwa kamati ya uongozi inaweza kujadili masuala ya kanuni.
Majibu ya Chenge yaliwanyanyua wabunge wote wa upinzani, huku Pauline Gekul (Babati Mjini) na John Heche (Tarime Vijijini) wakiomba mwongozo ambao Chenge alijibu kwa kurejea uamuzi wa Kamati ya Uongozi.
 Kutokana na wabunge hao kugoma kukaa huku wakipiga kelele, kujibiwa na wabunge wa CCM waliokuwa wakishangilia kwa mtindo wa kupiga meza, saa 10:50 jioni Chenge aliamuru askari wa Bunge kuwatoa wabunge hao.
Kabla ya uamuzi huo, Chenge aliamuru Lissu, Ester Bulaya (Bunda), Gekul na Godbles Lema (Arusha Mjini) kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kwa maelezo kuwa ndio walikuwa vinara wa vurugu hizo.
Hata hivyo, wabunge hao waligoma huku Lema akisimama na kuvua koti na tai, akisema kuwa hakuwa akizungumza chochote.
Baada ya Chenge kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, polisi wanane waliingia kuwatoa wabunge hao bila mafanikio, na kulazimika kuita polisi 18 waliokuwa wamevaa sare pamoja na wengine nane waliovaa kiraia.
Licha ya wingi wa askari hao ambao walizunguka eneo wanalokaa wabunge wa upinzani, walishindwa kuwatoa na kulazimika kuwaita askari tisa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuongeza nguvu.
Wabunge kadhaa walitolewa ndani ya ukumbi wa Bunge huku wakiwa wamebebwa juu juu na kuchaniwa nguo zao, kusababisha baadhi yao kurushiana makonde na askari hao.
Baada ya askari hao kufanikiwa kuwatoa nje, wabunge waliosalia ambao ni kutoka CCM waliendelea kujadili hotuba ya Rais, huku waandishi wa habari nao wakitakiwa kurejea ukumbini.
Kauli ya Ukawa
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi, Serikali ilibadili mjadala kutoka gharama za kurusha matangazo hayo na kuibuka na madai kuwa watumishi wa Serikali hawafanyi kazi kwa sababu ya kuangalia matangazo ya Bunge.
“Pia Serikali ilileta hoja kuwa wakati wa mchana wananchi hawatazami televisheni na usiku ndio wanakuwa na muda zaidi. Sisi tulipinga hoja hizo kwa kutambua kuwa huo ni mkakati maalumu wa Serikali na ulianza tangu wakati wa kampeni, sasa umefikia hatua ya kufungia vyombo vya habari,” alisema Mbowe.
“Walianza siku nyingi na hata kufikia hatua ya kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara. Uamuzi huu utawafanya wananchi kutosikiliza taarifa za Serikali.”
Alisema walirejea kwenye kikao cha Bunge jioni kwa nia ya kupinga uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo hayo kwa lengo la kuijulisha dunia juu ya kinachofanywa na Serikali ya CCM.
“Watu wanafukuzwa kazi bila kufuata taratibu, mfano ni mabalozi waliotakiwa kurudi nyumbani haraka. Huku ni kujenga misingi ya udikteta katika taifa. Mawaziri nao wanafukuza watu hovyo, wakuu wa wilaya ya mikoa nao, halafu  sisi tunasema ni majipu?” alihoji Mbowe.
“Tunalaani Serikali ya Magufuli kwa kutozingatia uhuru wa wananchi kupata habari, uhuru wa Bunge kusikilizwa. Tutapaza sauti ndani na nje ya Bunge. Hatuwezi kuruhusu mambo haya kuonekana ni utaratibu wa kawaida.”
Alisema kuna taarifa kuwa Serikali inahofia kujadiliwa kwa suala la Zanzibar, yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu,“Tutaonyesha upande wa pili wa Serikali ya Magufuli,” alisema.
 Alisema vyombo vya dola vinatumika kuziba haki na uhuru wa wananchi, kama majeshi yanavyotumika kudhibiti wananchi baada yakufutwa kwa uchaguzi Zanzibar.
“Sasa tumeonyeshwa kuwa Bunge ni pamoja na FFU, polisi na mbwa. Tulichokitaka ni mjadala wa kutetea wananchi kupata habari. Chenge kakimbia kiti na kuacha Bunge kuongozwa na askari,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa kama watashiriki katika kikao cha Bunge cha leo, Mbowe alisema: “Kesho (leo) tutaingia bungeni. Tambueni kuwa hata nyinyi (waandishi) mlifukuzwa. Ipo siku mtafukuzwa kabisa maana Serikali haitaki kuambiwa ukweli. Serikali ikifanya jema tutawapongeza, isipofanya jema tutasema.”
Alisema kuna wabunge wameumizwa kwa kipigo, kuibiwa saa, pochi na simu.
“Bunge kuendelea ni unafiki wa wabunge wa CCM. Asubuhi wakati tunashinikiza Bunge lijadili hoja hii, wabunge wa CCM walituandikia vikaratasi kutuunga mkono ila jioni wametugeuka,” alisema.
Baadhi ya waandishi waliojiwa na Mwananchi baada ya sakata hilo walisema inasikitisha kuona wanafanyiwa vitendo hivyo.
Kauli za wanahabari
Mwandishi wa gazeti la Mtanzania, Elias Msuya alisema: “Ni jambo la kusikitisha maana tumepewa vitambulisho kwa ajili ya kuandika habari za Bunge, lakini leo hii tunafukuzwa. Imeniuma sana.”
 Kwa upande wake mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Ibrahim Yamola ambaye aliporwa simu yake na askari baada ya kupiga picha, alisema: “Ni tukio la kusikitisha, ni kama tulizuiwa kufanya kazi yetu.”
Wakati huo huo, msemaji wa Bunge, Owen Mwandumbya amesema kuwa waandishi wa habari saba watarudishwa na hawataruhusiwa kuripoti habari za Bunge kwa kile kilichoelezwa kukiuka kanuni na taratibu za Bunge.
Hata hivyo, hakuwataja moja kwa moja waandishi hao wa habari na kusema sababu kubwa ni kugoma kutii maagizo ya kutotakiwa kwenye baadhi ya maeneo ya Bunge na zaidi wakati wa vurugu hizo.    
Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA

HILI NDILO BIFU KUBWA KATI YA RIHANA NA NICK MINAJ.