Sakata la Tegeta Escrow: Mtuhumiwa kinara wa kashfa ya rushwa Tanzania aandika barua ya kukiri makosa
Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Bw. Habinder Singh Seth ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa na kuomba msamaha.
Wakili wa Seth, Michaele Ngalo, ameiarifu Mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Oktoba 10.
Seth pamoja na mfanyabiashara mwenzake James Rugemalira, wanahusishwa na kashfa ya rushwa maarufu nchini Tanzania kama Tegeta Escrow, baada ya kulipwa mamilioni ya dola kutoka kwenye akaunti ya benki kuu ya nchi hiyo zilizohifadhiwa kutokana na mgogoro baina ya kampuni ya IPTL na Shirika la Kuzalisha na Kusambaza Umeme Tanzania (Tanzania).
Wawili hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 wanayodaiwa kuyatenda jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.
Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama hiyo Juni 19, 2017 na hadi sasa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Miongoni mwa mashtaka hayo ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi na kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya Dola milioni 22 na Shilingi za Tanzania bilioni 309.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 na wakili wake, Michael Ngalo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amethibitisha kuwa wamepokea barua ya Seth wanaifanyia kazi na majibu yatatolewa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 24, 2019.
Sakata la Escrow liliitikisa serikali ya awamu ya nne ya Tanzania chini ya Raisi Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2014 na mwanzoni mwa mwaka 2015 baada ya kamati maalumu ya Bunge kuchunguza tuhuma za rushwa.
Ripoti ya bunge ilipelekea maafisa kadhaa waandamizi wa serikali ikiwemo mawaziri na mwanasheria mkuu kupoteza nafasi zao.
Msamaha wa rais Magufuli
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli alitangaza msamaha Septemba 22, kwa watuhumiwa wa makosa hayo ambao wataandika barua za kukiri makosa, kuomba radhi na kukubali kulipa fedha wanazotuhumiwa kujipatia kinyume cha sheria.
Mashtaka ya uhujumu uchumi nchini Tanzania hayana dhamana, na watuhumiwa wake hkaa mahabusu mpaka kesi zao kuhukumiwa.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Tanzania, Biswalo Mganga, ambaye ndiye anaepokea barua hizo alibainisha kuwa mpaka kufikia Septemba 30, ofisi yake ilishapokea barua 467.
Jumla ya Shilingi bilioni 107 za Tanzania sawa na takribani dola milioni 4.6 zinatarajiwa kurejeshwa na watuhumiwa hao.
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura ni moja ya watu maarufu ambao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka hayo. Tayari maombi yake ya msamaha yamekubaliwa na kutoka mahabusu Jumatatu wiki hii. Wambura amekubali kulipa kiasi cha Shilingi za Tanzania milioni 100, kwa awamu na tayari ameshatoa milioni 20.
"DPP mfanye haraka, msichukue muda mrefu kupitia maombi hayo ili watu hawa warudi kwenye jumuiya zao. Ikichukua mwezi ama mwaka hata dhana nzima ya msamaha itaondoka," ameagiza rais Magufuli.
Toka aingie madarakani takribani miaka minne iliyopita Magufuli amejipambanua kwa kupigana dhidi ya rushwa na ufisadi.
Katika vita hiyo, vigogo kadhaa wa serikali walifutwa kazi kwa tuhuma za uzembe na rushwa.
Watu kadhaa pia wamefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na kesi nyingi kati ya hizo bado zinaunguruma.
"Najua wanateseka. Unaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli, inatia huruma na inaumiza. Najua wengine wanataka kuomba msamaha..." alisema Magufuli Septemba 22, wakati akitangaza msamaha.
Hata hivyo alionya kuwa kwa wale watakaoshindwa kuomba msamaha, waendelee kubanwa hata kama kesi zao zitachukua miaka 20.
Maoni
Chapisha Maoni