TMA YATAJA DAR KUPATA MVUA KUBWA ZAIDI!.............YASHAURI.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwepo kwa mvua zitakazoambatana na mawimbi makubwa baharini na upepo mkali kutokana na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo mbalimbali.
Taarifa hiyo iliyotolewa na mkurugenzi mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 10, 2019 imeeleza kuwa mifumo inaonyesha kuwa mvua za nje ya msimu zitaendelea kwa muda, hivyo amewashauri wakulima ukanda wa Kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, Arusha na Manyara wanaweza kuzitumia kuanza kilimo.
“Na hizi mvua za nje ya msimu mifumo inaonyesha zitaendelea kwa muda hivyo tunawashauri wakulima ukanda wa Kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, Arusha na Manyara wanaweza kuzitumia kuanza kilimo,” amesema Dkt. Kijazi.
Dkt. Agnes Kijazi amesema kuwa tangu kuanza kwa mvua zisizo za msimu ukanda wa Dar es Salaam umepata kiasi kikubwa cha mvua cha zaidi ya mililita 145 ambacho ni kiwango kikubwa kwa mvua hizo.
“Mpaka sasa ukanda wa Dar es Salaam tumesharekodi mvua za mililita zaidi ya 145 ni mvua kubwa pamoja na Pwani ya Kaskazini.”
Amesema maeneo ya Pwani ya Kusini mvua hizo zimeanza nje ya msimu kutokana na mgandamizo uliojitokeza uliosababisha kuongezeka kwa mvua katika ukanda wa Pwani.
Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha baadhi ya maeneo kujaa maji, kutopitika jambo ambalo limekuwa usumbufu kwa wananchi watembea kwa miguu na wanaotumia magari.
Maoni
Chapisha Maoni