Saudi Arabia: Wapenzi sasa kulala chumba kimoja cha hoteli Saudia
Wapenzi raia wa kigeni ambao hawajaoana sasa wanaweza kulala chumba kimoja cha hoteli nchini Saudi Arabia.
Hayo ni sehemu ya mabadiliko ya masharti ya kupata viza yaliyotangazwa hivi karibuni na taifa hilo ambalo limekuwa likiendeshwa na sheria za kihafidhina za dini ya Kiislamu.
Wanawake pia sasa wataruhusiwa kupanga vyumba vya hoteli peke yao.
- Kanda za siri za mauaji ya Khashoggi zafichuliwa
- Unalijua chimbuko la illuminati?
- Umoja wa mataifa unataka vita visitishwe Iraq
Wapenzi hapo awali walitakiwa kutoa uthipitisho wa kuwa wameoana kabla ya kupata chumba cha hoteli.
Mabadiliko hayo yanakuja katika kipindi ambacho serikali ya Saudia inajipanga kukuza sekta ya utalii nchini humo.
Vipi kuhusu pombe?
"Raia wote wa Saudia wanatakiwa kuonesha vitambulisho vya familia ama uthibitisho wa mahusiano wakati wa kukodi vyumba vya hoteli," ameeleza Kamishna wa Utalii na Urithi wa Taifa wa Saudia katika taarifa yake.
"Uthibitisho huo hata hivyo hautawahusu watalii raia wa kigeni. Wanawake wote, wakiwemo raia wa Saudia sasa ruksa wanaweza kupanga vyumba vya hoteli wakiwa peke yao, alimradi tu wawe na vitambulisho."
Mabadiliko hayo yanaeleza kuwa watalii wanawake si lazima wavae ushungi lakini wanategemewa kuwa watavaa kwa kujihifadhi vizuri.
Pombe ingali marufuku.
Nini kimesukuma mabadiliko hayo?
Kwa muda mrefu Saudia imekuwa ikionekana kama nchi yenye masharti magumu zaidi duniani. Sasa utawala wa Kifalme unajaribu kuiondosha picha hiyo kwenye mitazamo ya watu, hususani wawekezaji na watalii wa kigeni.
Mwanamfalme Mohammed bin Salman katika miaka ya hivi karibuni amejaribu kufanya mabadiliko katika nchi hiyo ambayo viongozi wa kidini wa kihafidhina ndio wamekuwa wakiamua nini kiwe sheria.
Mabadiliko hayo yamehusisha kuondolewa kwa marufuku ya wanawake kundesha magari, na kuwaruhusu wanawake kusafiri bila ya kusindikizwa ama kupata ruhusa ya mwanaume.
Hata hivyo mabadiliko yote hayo yamemezwa na mambo mengine yanayoendelea nchini humo ikiwemo mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.
Simon Calder, ambaye ni mhariri mwandamizi wa habari za utalii na safari wa gazeti la The Independent, amesema kulegeza masharti ya viza kutaleta ongezeko kubwa la watalii nchini humo.
"Kwa kufanya jambo lililokuwa na urasimu mkubwa kuwa jepesi kutafanya idadi ya watalii kuongezeka maradufu - mwanzoni, naona, watakuwa (watalii) wale wanaovutiwa na ulimwengu wa Kiarabu na urithi wake," Bw Calder ameieleza BBC.
Maoni
Chapisha Maoni