RAIS MAGUFULI NA WAZIRI MKUU WATOA MAJINA HADHARANI YA VIGOGO WALIOIFILISI NCHI..HII ORODHA INATISHA


Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imetaja majina ya kampuni 43 na wamiliki wa makontena 329 ambayo yalipitishwa bandarini bila kulipiwa na kufichuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita.
Aidha, TRA imesema imesimamisha kazi watumishi wake 35 wanaofanya kazi katika ngazi mbalimbali, wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika Geti Namba Tano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Philip Mpango alisema Mamlaka hiyo iliagizwa na Waziri Mkuu Majaliwa kuchukua hatua mara moja kwa kufuatilia na kubaini wamiliki wa Bandari Kavu (ICD) zilizohusika katika kashfa hiyo.
Alisema mbali na hilo walitakiwa kuwatambua wamiliki wa makontena hayo, bidhaa zilizokuwemo, kuwalipisha wahusika kodi iliyokwepwa pamoja na kuwachukulia hatua watumishi waliohusika na upotevu huo.
Dk. Mpango aliyataja makampuni hayo kuwa ni Lotai Steel Tanzania Ltd iliyokuwa na makontena 100, Tuff Tryes Centre Company 58, Binslum Tyres Company Ltd 33, Tifo Global Mart Company Limited 30, Ips Roofing Company Limited 20, Rushywheel Tyre Centre Co Ltd 12 na Kiungani Trading Co Ltd 10.
Makampuni mengine yaliyotajwa ni Homing International Limited (9), Red East Building Materials Company Ltd (7), Tybat Trading Co Limited (5), Zing Ent Ltd (4), Juma Kassem Abdul (3), Salum Link Tyres (3), Ally Masoud Dama (2), Cla Tokyo Limited (2), Farid Abdullah Salem (2), Salum Continental Co (2), Zuleha Abbas Ali (2) na Snow Leopard Building (2).
Wamiliki wengine wa makampuni ambayo yalikuwa na kontena moja moja ni Abdulaziz Mohamed Ally, Ahmed Saleh Tawred, Ali Amer, Ally Awes Alhamdany, Awadhi Salim Saleh, Fahed Abdallah Said, Hani Said, Hassan Husrin Suleyman, Humud Suleiman Humud, Kamil Hussein Ali na Libas Fashion.
Wengine ni Nassir Salehe Mazrui, Ngiloi Ulomi Enterprises Co Ltd, Omar Hussein Badawy, Said Ahmad Hamdan, Said Ahmed Said, Salumu Peculier Tyres, Sapato N. Kyando, Simbo Yonah Kimaro, Strauss International Co. Ltd na Swaleh Mohamed Swaleh.
Alisema kwa ujumla, makampuni hayo yalipitisha makontena 329 ambayo yaliondolewa kinyume cha taratibu kutoka ICD ya Azam inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa And Company Limited.
Dk. Mpango alisema bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo ni pamoja na matairi ya magari, samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa zingine mchanganyiko.
27 WALIOKAMATWA
Aidha, Dk. Mpango alisema watumishi 35 wa Mamlaka hiyo wanaofanya kazi katika vitengo mbalimbali wamesimamishwa kazi, wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika geti namba tano.
Alisema watumishi hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano huku akisisitiza kuwa mtumishi yoyote wa TRA atakayebainika kuhusika katika hujuma hiyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi kulingana na makosa atakayokutwa nayo.
Alisema TRA inaendelea kupanga safu ya watumishi wake ili kuthibiti upotevu wa malipo ya kodi na kwamba wanapitia upya taratibu za utoaji leseni kwa Bandari Kavu ili kuondoa mianya na kuweka udhibiti katika uondoshaji wa mizigo katika bandari zote na bohari za forodha.
“Pamoja na hatua hizi, TRA inafuatilia kwa kina ili kubaini mawakala wote wa forodha walioshiriki katika upotevu wa makontena hayo na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia leseni pamoja na adhabu zingine kwa mujibu wa sheria,” alisema Dk. Mpango
Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali ya awamu tano chini ya Rais John Magufuli ilibaini ukwepaji wa kodi kwa kutorosha makontena 329 ambayo yamenyima serikali kodi ya Sh. bilioni 80.
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade huku Jeshi la Polisi likiwashikilia maofisa kadhaa waandamizi wa Mamlaka hiyo akiwemo Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki.
Masamaki na wengine saba walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu jana.
CHANZO: NIPASHE

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ujerumani yanyakua Kombe la nne la Dunia

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA

HILI NDILO BIFU KUBWA KATI YA RIHANA NA NICK MINAJ.