WABUNGE WAGOMEA MILIONI 90 ZA MASHANGINGI,WATAKA ZIONGEZWE
Mwaka
2010, wabunge walilipwa Sh90 milioni kwa ajili ya ununuzi wa magari
hayo aina ya Toyota Land Cruiser (hardtop), ambayo ni vitendea kazi
vyao. Wabunge hutakiwa kulipa nusu ya fedha hizo wkati nyingine ni mchango wa Serikali.
Lakini
wakati gharama za maisha zikipanda huku thamani ya Shilingi ikiporomoka
kulinganisha na Dola ya Marekani na hivyo kusababisha bidhaa kupanda
bei, wabunge wamekataa kulipwa kiasi hicho cha fedha mwaka huu na badala
yake wanataka walipwe kulingana na bei ya sokoni ya magari aina hiyo.
Kwa
mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata, wabunge wanataka walipwe
Sh130 milioni ambazo wanasema ni bei ya magari hayo kwa sasa baada ya
kupanda bei.
Wakizungumza
na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya wabunge walisema
mara baada ya kujisajili bungeni kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la Kumi
na Moja, katibu wa chombo hicho, Dk Thomas Kashililah alifanya kikao na
wabunge wote ili kuwapa taratibu lakini pia kuwafahamisha stahili
wanazopaswa kupata kama wabunge.
“Katibu
alitujulisha kuwa tunapaswa kulipwa kiasi cha Sh300,000 kwa siku za
posho, lakini pia tutapewa Sh90 milioni kwa ajili ya mkopo wa gari ambao
nusu hutolewa na ofisi ya Bunge na kiasi kilichobaki tunapaswa kulipa
wenyewe,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Kwa
mujibu wa chanzo hicho, suala hilo liliibua mjadala na kusababisha
wabunge kuhoji iweje kiwango hicho kitumike katika Bunge la Kumi na
Moja, miaka mitano baada ya wabunge wa Bunge la 10 kupewa kiasi hicho.
“Unajua
magari tunayotakiwa kununua ni Toyota Land Cruiser Hardtop, na ukweli
sasa thamani ya magari hayo imepanda sana huwezi kuifananisha na mwaka
2010 wakati wa Bunge la 10,” alisema mbunge mmoja.
Wabunge hao walitaka walipwe kiasi cha Sh130 milioni kwa madai kuwa ndiyo bei ya sokoni ya magari aina hiyo.
Mbunge
wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest alikanusha habari hizo
akisema hawajakataa fedha hizo, lakini walisema thamani ya Dola imepanda
hivyo kusababisha thamani ya magari hayo kupanda pia.
“Hakuna
asiyejua kwamba thamani ya Dola imepanda na kwa kawaida kila Bunge
kunakuwa na ongezeko la Sh30 milioni. Mfano Bunge la Tisa walipewa
Sh60milioni la 10 wakapewa Sh90milioni, hivyo ilipaswa sasa iwe Sh
120mililioni ili kuendana na soko,” alisema mbunge huyo.
Alisema baada ya mazunguzo hayo ofisi ya Bunge iliahidi kulifanyia utafiti suala hilo na kwamba ingewajibu.
Lakini,
Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu alisema wabunge
wanapaswa kufahamu wapo kwa ajili ya wananchi na si kujilimbikizia mali.
“Kwa
mfano mimi siwezi kuchukua fedha za posho kwa ajili ya kikao. Nimepanga
kumuandikia barua Spika juu ya uamuzi wangu. Mshahara wangu unanitosha
kabisa,” alisema Kingu ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga
kabla ya kutolewa katika nafasi hiyo na kugeukia ubunge.
Akizungumzia
sakata hilo, katibu wa Bunge alisema masharti na vigezo vilivyotumika
mwaka 2010, ndivyo vinavyoendelea kutumika katika Bunge hili, na hivyo
hakuna kilichobadilika.
Dk
Kashililah alisema fedha za magari hayo hutolewa na Wizara ya Fedha
kama mkopo na wabunge wataulipia huku kiasi kingine wakipewa kama ruzuku
ya kununulia magari.
Hata hivyo hakutaka kuzungumzia kiwango halisi cha fedha zinazotolewa kwa wabunge hao.
Awali
naibu katibu wa Bunge, John Joel alisema jukumu la ununuzi wa magari ya
wabunge, lipo chini ya Serikali na siyo ofisi yake hivyo ni bora
wangeulizwa wenye jukumu hilo.
“Tunachofamu sisi mbunge anatakiwa apewe vitendea kazi likiwemo gari, lakini wanaohusika na hilo ni Serikali,” alisema.
“Sisi
huwa tunawahudumia jimbo allowance (posho) kwa ajili ya kuhudumia ofisi
ya mbunge na kununua mafuta ya gari,” alisema Joel bila kutaja kiwango
cha posho hiyo.
Alisema
ofisi ya Bunge hushauriana na Serikali namna ya kutoa huduma kwa
wabunge na kwamba kwa jinsi anavyofahamu, mpaka jana watunga sheria hao
walikuwa hawajapewa fedha yoyote ya kununua magari kwa awamu hii, hivyo
wanasubiri utaratibu.
Wakati
Joel akisema Serikali ndiyo inahusika, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Ombeni Sefue aliurudisha mpira kwenye ofisi hiyo ya Bunge, akisema
uongozi wa chombo hicho ndio uulizwe.
Katika
kukusanya fedha za kuwezesha kutekeleza mipango ya Serikali na ahadi
alizotoa wakati wa kampeni, Rais John Maguguli alitangaza hatua
mbalimbali za kudhibiti matumizi, na akawaeleza wabunge mwishoni mwa
wiki kuwa hataweza kufanikiwa iwapo hatapata ushirikiano wao.
Katika
kuonyesha kuwa anatoa kauli thabiti, Dk Magufuli aliagiza fedha ambazo
zilichangwa na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya hafla za
kuwapongeza wabunge, zielekezwe kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwenye
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tayari
Rais ameshafuta safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu baada ya
mtu anayetaka kusafiri kutimiza masharti kadhaa, likiwamo linalomtaka
aeleze faida ya safari yake na kama iwapo hatasafiri, nchi itaathirika
vipi.
Maoni
Chapisha Maoni