RAIS MAGUFULI AWASILI KUHUTUBIA BUNGE,WAZIRI MKUU HADHARANI,UKAWA HALI TETE



Rais wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli, amewasili jana hapa Dodoma tayari kwa kulihutubia na kulizindua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Magufuli, katika hotuba yake, anatazamiwa kugusia mwelekeo wa Serikali yake ya awamu ya tano na nini kinalengwa kufanyika. Rais Magufuli anatazamiwa kukumbushia utekelezwaji wa Ilani ya CCM ya 2010-2015 na kutaja vipaumbele vya Ilani ya CCM ya 2015-2020 na jinsi vitakavyotekelezwa.
Hadi sasa, Wabunge wanaotokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na vyama vya CHADEMA,CUF na NCCR-Mageuzi wameshawasili kwa wingi hapa Dodoma na hata jana wote waliopo hapa Dodoma walishiriki kupiga kura za kumchagua Spika wa Bunge: Job Yustino Ndugai. Ikumbukwe kuwa jana, kura zote za Wabunge ziligawanywa kwa wagombea wa CCM na CHADEMA tu kwakuwa wagombea wengine sita hawakupata kura.
UKAWA wanasemwa kuwa wamejipanga kugomea hotuba ya Rais Magufuli kwa ima kutoingia Bungeni wakati wa hotuba hiyo au kuingia na kupiga kelele. Lakini, taarifa za kiintelijensia katika viunga vya Dodoma hazijathibitisha yasemwayo. UKAWA bado hawasomeki. Wanaendelea na vikao vyao vya siri kwa umakini mkubwa huku wakiwa wamoja kuliko muda wowote tangu UKAWA uundwe. UKAWA na CCM wataanza mtanange wao wa hoja za haja hivi karibuni Bungeni Dodoma.
Kila kitu kipo tayari. Kila mtu yupo tayari. Kila chombo cha habari kipo tayari. Wananchi wako standby. Kumsikiliza Rais, kushuhudia Waziri Mkuu mpya, Naibu Spika mpya na mnyukano usio na mfano katika kuendesha Taifa letu kidemokrasia. Hapa CCM, pale UKAWA. Hapatoshi Dodoma!

Mzee Tupatupa wa Lumumba (kwasasa Dodoma)

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Nani aligharamia ukarabati wa kifahari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA