Kingunge amtolea uvivu Nape Nnauye
Na Sharon Sauwa
Kwa ufupi
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana,
Kingunge (pichani), ambaye hivi karibuni aliweka bayana kumuunga mkono
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania urais,
alisema hakubaliani na kauli ya Nape kuwa wagombea wasioridhika na
uamuzi wa Kamati Kuu (CC), hawawezi kukata rufaa kwa sababu ya muda kuwa
mfupi.
Dodoma. Mwanasiasa mkongwe wa
CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru amemshukia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye kwa kauli zake alizodai zinaminya demokrasia na
kwamba CCM haiwezi kusimama wanapopambana wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
jana, Kingunge (pichani), ambaye hivi karibuni aliweka bayana kumuunga
mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania
urais, alisema hakubaliani na kauli ya Nape kuwa wagombea wasioridhika
na uamuzi wa Kamati Kuu (CC), hawawezi kukata rufaa kwa sababu ya muda
kuwa mfupi.
Alisema CCM imeweka utaratibu wa wanachama kudai haki zao ndani ya chama, pindi wasiporidhishwa na uamuzi wa vikao vya chini.
Alisema mwaka 2005, mgombea wa nafasi ya urais,
John Malecela alikata rufaa katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) baada
ya jina lake kutopelekwa.
“Aliyekuwa mwenyekiti wa chama wakati ule Mkapa
(Benjamin), alikubali baada ya kushauriana na wenzake kwa sababu haikuwa
zawadi, bali ni haki yake,” alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya kujielezea mbele ya
NEC na wajumbe kuulizwa, walikubali kuwa majina matano yaliyoletwa na CC
yanatosha.
“Kufikiria kwamba mtu akose haki kwa sababu ya kukosa muda huko ni kuwakosesha watu haki,” alisema.
Kingunge alisema amani na utulivu ni mambo yanayojengwa kwa haki na lazima imani ijengwe na viongozi.
Alisema lugha za kibabe ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi huku chama kikaa kimya ndizo zinazowatia watu shaka.
“Sasa hivi kumekuwa na nguvu kubwa ya kupambana
ndani ya chama kuliko wapinzani… nyumba ikigawanyika haiwezi kusimama na
CCM haiwezi kusimama inapopambana yenyewe kwa yenyewe,” alisema.
Alisema kukiwa kuna jitihada za kunyima haki watu, kunaweza kusababisha machafuko.
“Asitokee mtu akadhani kuwa nchi ni yake pekee
yake, sitaki kusema kwa sababu matokeo yake mnayajua. CCM ni yetu sote
hata sisi tuliokuwapo tangu zamani,” alisema. “Ukisema wagombea
hawataweza kukata rufaa unapotosha misingi, kwa nini unataka kuminya
haki hiyo sasa? Ingekuwa wakati wetu na Mwalimu (Julius Nyerere), mtu wa
namna hiyo tungemvua uongozi.”
Maoni
Chapisha Maoni