Yajuwe makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati na Afrika
Wakati dunia zamani ikililia zaidi kwa maradhi, njaa na umasikini, kilio kikubwa zaidi sasa kimekuwa ni wimbi la makundi ya siasa kali ambayo hujihusisha na uhalifu na ugaidi kwa jina la dini.
Ifuatayo ni orodha ya makundi hayo yanayopatikana kwenye eneo la Mashariki ya Kati, Ghuba na Afrika.
Dola la Kiislamu Iraq na Syria (ISIS)
Wafuasi wengi wa kundi hili ni waumini wa madhehebu ya Sunni wenye msimamo mkali wa kidini. ISIS imepata nguvu kwa mda mfupi tu na kueneza ushawishi wake katika maeneo yote wanayoyadhibiti nchini Syria na Iraq. Muongozo na nadharia yao ni kifupisho cha jina lao - ISIS au Dola la Kiislam kuanzia Iraq, Syria na katika eneo la Sham.
Lengo lake ni kubuni dola kubwa la Kiislam litakaloziunganisha Syria, sehemu ya Iraq, Lebanon na sehemu kubwa ya Palestina na Jordan. Kundi hili linasemekana kuwa na msimamo mkali zaidi kuliko hata al-Qaida. Sehemu kubwa ya operesheni zake zinagharimiwa na wafadhili binafsi kutoka mataifa ya Ghuba, hasa Qatar na Saudi Arabia.
Vyenzo vyengine vinavyowapatia fedha ni visima vya mafuta kaskazini ya Syria na hongo. Wataalamu wanakadiria kundi hili la kigaidi lina wapiganaji wasiopungua 10, 000 na kwamba limejivunia umashuhuri mkubwa zaidi katika ugomvi kati ya jamii ya Sunni walio wachache na Shia wengi nchini Iraq. Zaidi ya hayo, ndani ya kundi hilo muna pia wanamgambo kadhaa wa kigeni waliojitolea kupigana jihadi, baadhi yao wakiwa ni wale waliosilimu.
Al-Nusra Front la Syria
Al-Nusra linaangaaliwa kuwa ni tawi la al-Qaida na jina lake linamaanisha "Waungaji mkono wa umma wa Syria". Linatajikana kuwa kundi muhimu kabisa la waasi nchini Syria. Malengo yao ni pamoja na kuundwa kwa dola la Kiislamu nchini Syria na katika eneo la Mashariki la Bahari ya Kati.
Al-Nusra linakadiriwa kuwa na wafuasi kati ya 5,000 na 7,000 wanaokutikana zaidi katika eneo la kaskazini mwa Syria, ingawa hivi karibuni lilitangaza utiifu wake kwa hasimu wake wa zamani, ISIS.
Boko Haram la Nigeria
Jina la kundi hili linamaanisha kwa ufupi kuwa "elimu ya Magharibi ni dhambi". Wanapigana kwa sehemu kubwa kaskazini ya Nigeria na wanapigania utawala wa Sharia ya Kiislamu kote nchini Nigeria. Wafuasi wake wanajulikana zaidi kutokana na utekaji nyara. Umaskini uliokithiri na ukosefu ajira kaskazini mwa Nigeria unawarahisishia kazi viongozi wa Boko Haram kuwasajili wanamgambo wapya.
Vikosi vya usalama vya Nigeria vina pata shida ya kukabiliana na magaidi hao wenye silaha za kila aina. Tangu mwaka 2003 ,mashambulizi yamekuwa yakifanyika dhidi ya vikosi vya usalama, idara za serikali, makanisa na shule na maelfu ya watu kuuliwa. Katika miezi minne ya mwanzo ya mwaka 2014 pekee,watu waiopungua 4,000 wameuwawa kutokana na mashambulizi ya Boko Haram.
Al-Shabab la Somalia
Harakat al-Shabaab al-Mujahideen (HSM) au al-Shabaab (Vijana) kwa ufupi ni kundi la wanamgambo wa Kiislamu lililoundwa kati ya mwaka 2004 na 2006 nchini Somalia, wakati nchi hiyo ikiwa tayari imeshazama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kundi hilo linapigania kuundwa kwa dola la Kiislamu katika Pembe ya Afrika. Nadharia yao ya itikadi kali ya dini ya Kiislamu haitambui mipaka. Wanafanya mashambulizi hivi sasa katika eneo lote la Afrika Mashariki -mfano katika mji mkuu wa Kenya ambako mashambulizi yake katika jengo la maduka makubwa la Westgate Septemba 2013 liliangamiza maisha ya zaidi ya watu 60.
Al-Shabaab wanadhibiti sehemu kubwa ya eneo la kati na kusini la Somalia. Wakuu wa kundi hilo, wengi wao wakiwa raia wa kigeni, wanashadidia kushirikiana na al-Qaida katika kuwapatia mafunzo wanamgambo. Zaidi ya hayo, kundi hilo lina mafungamano na Boko Haram.
Ansar-al-Sharia la Libya na Tunisia
Wenyewe wanajiita "Wafuasi wa Sharia ya Kiislamu" na kundi hili lina makao yake nchini Libya na Tunisia. Makundi madogo madogo ya Ansar-al Sharia yanakutikana pia kwenye mataifa mengine ya Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini. Lengo lao ni kuanzisha sheria ya dini ya Kiislamu.
Ngome ya Ansar-al Sharia, tawi la Libya, ipo Benghazi, ambako ni kitovu cha uasi uliokuja kumuondoa madarakani Muammar Gaddafi.
Kundi hilo linabebeshwa jukumu la mashambulizi dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, tarehe 11 Septemba 2012, ambayo yaliuwa watu wanne, ikiwa ni pamoja na balozi wa Marekani nchini Libya. Ansar-al Sharia linasemekana kuwa na mafungamano na al-Qaida, ingawa wenyewe wanakanusha dhana hizo.
Hizbullah la Lebanon
Kundi la wanamgambo wa Hizbullah nchini Libnan limeundwa mwaka 1982. Wanajipatia uungaji mkono kutoka mashirika na taasisi za madhehebu ya Shia nchini Iran na Syria. Tawi la kijeshi la kundi hilo linaangaliwa nchini Marekani na katika nchi za Umoja wa Ulaya kuwa ni kundi la kigaidi. Waamgambo wake wanapigana upande wa vikosi vya Rais Bashar al-Assad nchini Syria.
Hamas la Palestine
Vuguvugu la Kiislamu la Hamas limeundwa mwaka 1987. Hilo ni tawi la Chama cha Udugu wa Kiislam katika Palestina. Baada ya Fatah, chama cha kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina Mahmoud Abbas, Hamas ni kundi la pili muhimu linalowawakilisha Wapalestina.
Kinyume na Fatah, Hamas hawaitambui Israel. Lengo lao ni kuiona dola la Israel linateketezwa. Na ili kulifikia lengo hilo, wanatumia mbinu za kigaidi. Katika miaka ya '90, walifanya mashambulizi kadhaa ya kuyatolea muhanga maisha nchini Israel.
Tangu mwaka 2007, Hamas ndio wanaotawala katika eneo la Gaza katika wakati ambapo Fatah wanatawala katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Hivi karibuni, Fatah na Hamas wamesikilizana na kuunda serikali ya umoja. Israel imeanza kuwaandama na kuwakamata wafuasi wa Hamas, tangu walipotekwa nyara vijana watau wa Kiisraeli.
Al-Qaida - gaidi wa ulimwengu
Al-Qaida wanajulikana kama mama wa makundi yote ya jihadi ulimwenguni. Jina lake linamaanisha "msingi" ama "chanzo kikuu." Ndilo kundi lililopanga mashambulizi ya Septemba 11 2001 dhidi ya Marekani. Lengo lake ni kusimamisha dola la Kiislamu ambalo litayajumuisha mataifa yote ya Waislamu na waumini wa dini hiyo.
Baada ya kifo ya kiongozi wake, Osama bin Laden, al-Qaida sasa inaendeshwa na Aiman al-Zawahiri, ambaye ni mzaliwa wa Misri. Hivi leo, mtandao huo una matawi mengine kadhaa yanayojitambulisha nao katika mataifa mbalimbali duniani, kama vile al-Qaida ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika (AQIM), ambayo inaendesha harakati zake kutokea Algeria hadi Mali, na pia tawi lake la Yemen, ambako ni kitovu cha wapiganaji wa jihadi.
Maoni
Chapisha Maoni