Mbinyo dhidi ya Urusi waongezeka
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema suala la vikwazo vipya dhidi ya Urusi linaweza kurudishwa kwenye ajenda kama kasi ya kufanikisha hali ya utulivu nchini Ukraine haingozeki.
Katika hotuba hiyo aliyoitoa bungeni Kansela Merkel amempongeza rais wa Ukraine Petro Poroshenko kwa hatua kutoa wito wa pamoja wa kusitisha mapigano na wapiganaji waasi wanaoegemea upande wa Urusi na kusema uamuzi wa rais wa Urusi Vladimir Putin wa kujizuia kuingilia katika mgogoro huo kisaikolojia ni muhimu.
Lakini Kansela Merkel aliongeza kusema kuwa bado kuna hali ya hatari miongoni mwa vikosi vya Ukraine pamoja na wito wa kusitisha mapinago na utekelezaji wake umekuwa wa taratibu sana. Suluhu ya kisiasa ni muhimu lakini kama hakuna kinachojidhihirisha, vikwazo vitarejeshwa katika meza ya ajenda.
Hatua za Urusi kuhusu Ukraine
Katika hatua nyingine bunge nchini Urusi limepiga kura kufuta nguvu yake iliyotoa Machi kwa rais Putin kuamuru jeshi la taifa hilo kuingia nchini Ukraine. Kwa mujibu wa mbunge mmoja mwandamizi katika bunge la Ukraine hatua hiyo itazamwe kuwa inatokana na utashi wa rais Putin mwenyewe katika kufanikisha jitihada za kupatikana amani. Kura imeungwa mkono wa wabunge 153, na kura moja tu, ndiyo iliyopinga.
Wakati kukiripotiwa hatua hizo ndani ya Urusi, huko Brussel, mkuu wa Umoja wa Kujihami wa NATO, Anders Fogh Rasmussen ametoa taarifa yake kuhusu vitendo vya Urusi. "Hatuoni ishara yoyote kama Urusi inaheshimu wajibu wake kimataifa. Kwa hivyo leo hii tutapitia upya uhusiano wetu na Urusi. Na kutoa uamuzi wa nini cha kufanya baadae"
NATO tayari imekwisha simamisha shughuli zake na Urusi kufuatia taifa hilo kulitwaa eneo la Ukraine la Crimea ingawa pia imweka milango wazi kwa mawasiliano yake ya kisiasa ya ngazi ya juu wazi baina ya pande hizo mbili.
Nae waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, William Hague amewasili katika mkutano huo wa NATO, na kuonya kwamba uungaji mkono wa vikwazo dhidi ya Urusi utaongezeka kama taifa hilo halitafanya jitihada ya kumaliza mgogoro mashariki mwa Ukraine na kuunga mkono mpango wa amani wa rais Petro Poroshenko. Hatua kama hiyo imehimizwa pia na Marekani. Waziri wa Fedha wa Marekani Jacob Lew (Lyu)alisema wazi kabisa kuwa Urusi itapata adhabu zaidi kama itaendelea kuwaunga mkono wanamgambo wanaoipinga serikali. Lew alisisitiza ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na taifa lake baada ya kukutana na mwenzake wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble.
Maoni
Chapisha Maoni