BABU SEYA, PAPII KOCHA WAMLILIA JK


Wanamuziki wa Bendi ya Wafungwa, Nguza Viking ‘Babu Seya’ (kulia) na mwanaye Johnson Nguza "Papii Kocha’ (wa pili kulia) wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani, wakitumbuiza na wenzao katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ibrahim Yamola. 
KWA UFUPI
  • Nguza na mwanaye Papii walitoa ombi hilo kupitia wimbo wakati wakitumbuiza katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wanamuziki Nguza Viking na Papii Kocha wanaotumikia kifungo cha maisha jela, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete awasamehe kwa makosa waliyofanya.
Nguza na mwanaye Papii walitoa ombi hilo kupitia wimbo wakati wakitumbuiza katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.
Ombi hilo waliliwasilisha kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo ambapo Nguza maarufu Babu Seya na mwanawe, Johnson Nguza (Papii Kocha), walitumbuiza wakiwa na Bendi ya Wafungwa. Walimwomba Waziri Chikawe kufikisha ombi lao kwa Rais Kikwete.
Babu Seya na Papii Kocha walitoa burudani hiyo huku wakighani mashairi yenye ujumbe wa kuomba Rais awasamehe, hali iliowafanya mamia ya watu waliofurika kwenye hafla hiyo kutulia kimya, wengine wakilengwa na machozi.
Akiimba huku akitabasamu, Papi Kocha alikuwa akionyesha mikono ya kuomba msamaha na kusema: “Kosa gani sisi tusilosamehewa; vifungo vya maisha, miaka 30 gerezani havifundishi.”
“Waziri Chikawe tunaomba umfikishie Rais Jakaya Kikwete ombi letu, mwambie atusamehe. Hata Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini Yesu alimsamehe kwa nini sisi….,” alisikika akiimba Papi Kocha na baadhi ya wananchi waliohudhuria uwanjani hapo wakiinamisha vichwa chini na wengine kutokwa na machozi.
Akijibu ombi hilo wakati akiwahutubia wananchi Waziri Chikawe alisema: “Nimesikia maombi yenu, yamefika na nitajitahidi kuyafikisha kwa Rais Kikwete.”
Chikawe akijibu ombi hilo alisema “Mtu akishatumikia kifungo kwa miaka saba au 10 gerezani nina hakika kama ana moyo na nafasi ya kuacha, atakuwa amebadilika hivyo anaweza kupewa msamaha.”
Baadaye Chikawe alitembelea mabanda ya maonyesho na Bendi ya Wafungwa ikipewa tena nafasi ya kutumbuiza. Babu Seya aliimba wimbo maarufu wa  ‘Seya tucheze wote’ na umati wa watu kutoka kwenye mabanda ya maonyesho na kumiminika jukwaani kucheza wakiwamo askari magereza na wakishangilia jambo lililowafanya askari kuzuia bendi hiyo kuendelea kutumbuiza.
Awali, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Minja  alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Magereza katika kutekeleza majukumu ya jeshi hilo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Nani aligharamia ukarabati wa kifahari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA