DUH! SIKIA SERA ZA RAISI WA BRAZILI DHIDI YA KOMBE LA DUNIA:
KOMBE LA DUNIA 2014
Rais wa Brazil atetea maandalizi ya Kombe la Dunia
Rais Dilma Rousseff wa Brazil ametetea maandalizi ya serikali yake ya michuano ya soka Kombe la Dunia ambayo yamekuwa yakiandamwa na shutuma ya kuchelewa kwa maandalizi hayo pamoja na kupanda kwa gharama.
Wakati Brazil ikiwa inaharakisha kukamilisha viwanja vya kuchezea kabumbumbu na kukabiliana na wimbi la maandamano dhidi gharama zinazotumika kabla ya kuanza kwa michuano hiyo hapo tarehe 12 mwezi wa Juni ,Rousseff kwa kiasi fulani amelilaumu Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA kwa kuongezeka sana gharama za kuandaa michuano hiyo ya soka Kombe la Dunia lakini amesema fedha zilizotumika zitaacha nyuma urithi wenye manufaa.
Kiongozi huyo wa sera za mrengo wa shoto, ambaye anawania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa mwezi wa Oktoba, amesema FIFA ilikuwa imeihakikishia Brazil kwamba viwanja vya michuano hiyo vitajengwa kwa kutumia fedha za sekta binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa chakula cha jioni hapo Jumanne katika kasri la rais mjini Brasilia Rousseff amesema serikali hatimae ilikuja kutanabahi kwamba uwekezaji wa sekta binafsi hauwezi kugharamia hata nusu ya kiwanja na kwa hiyo ikabidi kugharamia yenyewe takriban gharama zote.
Amesema atazishauri nchi zitakazokuwa wenyeji wa michuano huyo huko kipindi cha usoni "kuwa waangalifu sana kuhusu chanzo cha wajibu" wakati wanaposaini makubaliano na FIFA.
Manufaa kwa Brazil
Rais Dilma Rousseff wa Brazili akiwa na wahandisi wakati alipoutembelea uwanja wa Itaquerao mjini Sao Paulo.
Amesisitiza kwamba sehemu kubwa ya gharama za wananchi zinazotumika kwa ajili ya michunao hiyo ni kwa manufaa ya Brazil kwa kuzingatia kipindi cha muda mrefu na sio tu kwa ajili ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Amesema kuandaa michuano hiyo kumechochea miji mingi kuingia katika miradi ya usafiri wa umma inayohitajika mno juu ya kwamba amekiri mingi ya miradi hiyo haitokamilika kabla ya michuano hiyo ya soka Kombe la Dunia.
Serikali ya Brazil imekuwa ikikabiliwa na wimbi la maandamano kupinga matumizi ya zaidi dola bilioni 11 kwa ajili ya michuano hiyo, fedha ambazo wakosoaji wanasema zilipaswa kutumika kushughulikia mahitaji ya dharura katika fani kama vile elimu,afya na usafiri.
Mwaka mmoja uliopita waandamanaji milioni moja walijazana mitaani wakati wa michuano ya Kombe la Mabara.Maandamano hayo mara nyegine yaligeuka kuwa ghasia na kuzusha hofu ya marudio yake kwa michuano hii ya Kombe la Dunia mwaka huu.
Akionekana mtulivu wakati akipata mlo wa jioni na waandishi wa habari,Rousseff amesema maandamano yataruhusiwa wakati wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia ili mradi yanakuwa ya amani na hayavurugi michuano hiyo.
Amesema "Tunahakikisha kikamilifu usalama wa wananchi."
Rais na shabiki wa soka
Brazil bado iko mbioni kukamilisha viwanja vyake vitano kati ya 12 vitakavyokuwa wenyeji wa michuano hiyo kikiwemo Corinthia Arena cha mji wa Sao Paulo ambao ndiko kutakapofanyika pambano la ufunguzi lakini bado havikuwekwa viti vyote.
Waandalizi wamefuta miradi mengine mingi ya miundo mbinu ambayo iliahidi hapo awali kuanzia ujenzi wa barabara hadi treni za mwendo wa kasi na zile za chini ya ardhi.
Lakini uwanjani Brazil inaonekana iko tayari kulifunguwa dimba hapo Jumanne baada kuichapa Panama mabao 4-0 katika mchezo wa kirafiki.
Rousseff mwenye umri wa miaka 66 ni dhahir alikuwa amefurahishwa na ushindi huo na kuahidi kuendelea kuwa na matumaini makubwa kwa kueleza kwamba ana imani na fursa iliokuwa nayo Brazil katika michuano hii.
Migomo yafutwa
Wakati huo huo serikali yake inaonekana kuwa imeweza kuzima tishio la mgomo wa polisi wa serikali kuu wakati wa michuano hiyo.
Migomo ya polisi ya hivi karibuni na tishio la kufanyika kwa migomo zaidi wakati wa michuano ya Kombe la Dunia ilikuwa ni miongoni mwa changamoto kubwa kabisa zenye kuisumbuwa serikali.
Lakini polisi ilitangaza kuwa imefikia makubaliano ya kuongezewa mishahara yao kwa asilimia 15.8 ili nayo itowe ahadi ya kutofanya migomo katika miezi inayokuja.Chama cha wafanyakazi wa polisi wa serikali kuu kimesema polisi katika mji mkuu wa Brasilia wamekubali pendekezo hilo ambalo litapigiwa kura katika majimbo yote 26 ya Brazil hivi karibuni.
Walimu katika mji wa Sao Paulo nao pia wamemaliza mgomo wao wa siku 42 baada ya kupatiwa nyongeza ya asilimia 15.4 kwa mishahara yao kuanzia mwezi wa Mei mwaka 2015.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman
Maoni
Chapisha Maoni