JE! WAJUA MAZOEZI HUIMARISHA TENDO LA NDOA HATA KWA WAZEE?
KWA UFUPI
Ripoti moja ya utafiti juu ya faida ya kufanya mazoezi katika kuimarisha nguvu za kiume Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kike na Uzazi, hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Y. Kapona, ana haya ya kusema:
Naendelea kujibu maswali yaliyoulizwa katika mada hii iliyoanzia wiki iliyopita na leo nitafafanua juu ya mazoezi ambayo ni muhimu kumwezesha mtu kuwa na uwezo mzuri wa kufanya tendo la ndoa.
Mwili unapokuwa katika hali nzuri, huimarisha nguvu za tendo hilo. Kukosa hamu au nguvu ya kufanya tendo la ndoa kwa wanaume na wanawake hutokana na mambo mengi.
Moja ya mambo hayo ni maisha ya kisasa ambayo yamerahisishwa na teknolojia inayosaidia watu wengi hasa mijini kufanya kazi bila ya kutoka jasho, kutazama televisheni kwa muda mwingi na kusafiri kwa kutumia vyombo kama vile magari, pikipiki na treni.
Kukua kwa teknolojia na uchumi katika karne hii nako kumesababisha matumizi makubwa ya vyakula visivyo kuwa na ubora kama vile vya mafuta, sukari, chumvi na kemikali nyingi.
Maisha ya aina hiyo yanasababisha matatizo mengi kiafya ikiwemo unene au uzito uliopitiliza. Mafuta mengi mwilini pia husababisha lehemu ambayo huweza kusababisha maradhi ya moyo na kisukari
Mambo yote haya kwa upande mwingine yanachangia kupunguza hamu na nguvu za kufanya tendo la ndoa, hasa kwa watu wasiofanya mazoezi au kazi za kutoka jasho.
Ili kulikabili tatizo la upungufu wa hamu na nguvu ya kufanya tendo la ndoa, lazima wanaume na wanawake wajifunze namna viungo vyao vya uzazi vinavyofanya kazi.
Wajifunze pia sababu zinazosababisha upungufu wa hamu na nguvu za kufanya tendo la ndoa.
Kinamama wanatakiwa waende mbali zaidi kwa kujifunza namna ya kuwasaidia waume zao kukabili tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.
Zaidi ya hayo, elimu ya kujua namna ya kufanya mazoezi ya viungo au kazi za kutoka jasho ni muhimu kuwezesha kuponya maradhi ya kukosa hamu na nguvu za tendo la ndoa.
Kufanya mazoezi ya viungo au kufanya kazi za kutoka jasho kama kulima au kutembea kwa miguu kunaimarisha nguvu ya mwili na akili.
Mazoezi husaidia mtu nguvu na hamu yake ya kufanya tendo la ndoa kubaki imara hata kama ana umri mkubwa.
Maoni
Chapisha Maoni