Iraq yapambana kuikombowa Tikrit
Vikosi vya Iraq vikisaidiwa na helikopta za mashambulizi vimeanzisha operesheni mapema Jumamosi (28.06.2014) ya kuukombowa mji wa kaskazini wa Tikrit kutoka mikono ya wanamgambo wa Kisunni ambao wameuteka hivi karibuni.
Baada ya kushuhudia sehemu kubwa ya ardhi ikinyakuliwa na wanamgambo hao kutoka kwenye mikono ya serikali,jeshi limekuwa mbioni kutaka kuonyesha operesheni hii iliyoanza kabla ya alfajiri kuwa ni hatua muhimu yenye kulirudisha jeshi kwenye hatua za mashambulizi.Jeshi hilo limesema kwamba operesheni hiyo imejumuisha makomandoo, vifaru na helikopta halikadhalika wapiganaji wa Kisunni wenye kuiunga mkono serikali na Washia waliojitolea.
Wakaazi wa Tikrit wameripoti kuwepo kwa mapigano kwenye viunga vya mji huo na kwa upande wa kusini lakini kiwango cha mapigano hayo hakikuweza kufahamika mara moja.
Jawad al- Bolani afisa wa usalama katika Kikosi cha Operesheni hiyo cha Saalahuddin amesema lengo la kwanza ni kuukombowa mji wa Tikrit alikozaliwa dikteta wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein na mojawapo ya miji miwili mikubwa kutekwa na kundi lililojitenga na Al Qaeda linalojitambulisha kama Dola la Kiislamu la Iraq na Sham na wanamgambo wa Kisunni wanaowaunga mkono.Amesema hakuna muda maalum uliowekwa kuikamilisha operesheni hiyo.
Mashambulizi yaanza alfajiri
Luteni Generali Qassim amesema helikopta za kivita zilifanya mashambulizi ya anga kabla ya alfajiri kwa waasi ambao walikuwa wakiwashambulia wanajeshi wa serikali katika kitivo cha chuo kikuu kwenye viunga vya kaskazini vya mji huo wa Tikrit.Habari kuhusu maafa hazikuweza kupatikana mara moja.
Vikosi vya serikali viliweka daraja kwenye kitivo hicho kikubwa hapo Ijumaa baada ya kusafirishwa kwenye eneo hilo kwa helikopta.
Afisa wa usalama wa ngazi ya juu akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema kumekuwepo mapigano ya hapa na pale karibu na chuo kikuu cha Tikrit halikadhalika kusini mwa mji huo.Amesema vikosi vya Iraq ambavyo vimekuwa vikisonga mbele kwa taabu kaskazini kuelekea Tikrit kutoka mji wenye maeneo takatifu wa Samarra.
Baadhi ya wakaazi wameshuhudia moshi mweusi ukifoka kutoka jengo la rais lilioko ukingoni mwa Mto Tigris baada ya kushambuliwa na helikopta za kijeshi.
Mji wa Tikrit umehamwa
Mkaazi mwengine wa Tikrit Muhanad Said al-Din amesema waakazi wameukimbia mji huo hivi karibu kwa kuepuka mapambano hayo yaliokuwa yakitarajiwa kati ya vikosi vya serikali na waasi.
Amesema watu wachache waliobakia wanahofia uwezekano wa kuzuka kwa vitendo vya kulipiza kisasi vya wanamgambo wa Kishia wanaoandamana na jeshi.Ameongeza kusema " Sisi raia wenye amani hatutaki kuwa wahanga wa mapigano hayo."
Mji huo unaelezwa kuwa umekuwa hauna maji wala umeme tokea Ijumaa.
Jeshi la Iraq pia limefanya mashambulizi matatu ya anga katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Mosul mapema Jumamosi ambapo shambulio moja lililenga eneo la kibiashara ambalo halikuwa na shabaha za kijeshi.
Wanamgambo hao wa Dola la Kiislamu la Iraq na Sham wameyateka karibu maeneo yote yanayokaliwa na Wasunni wengi kuanzia magharibi na kaskazini kutoka Baghdad hadi kwenye maeneo ya mipaka na Jordan na Syria.
Kurudisha imani
Jeshi kubwa la Iraq ambalo limepatiwa mafunzo na zana za kivita na Marekani liliingia mitini kutokana na mashambulizi hayo ya waasi na kuondosha morali na imani ya wananchi juu ya uwezo wa jeshi hilo kudhibiti kusonga mbele kwa waasi hao ukiachilia mbali kuyakombowa maeneo waliyoyateka.Iwapo operesheni hiyo ya Tikrit itafanikiwa itasaidia kurudisha kiwango fulani cha imani kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Pia itampa nguvu Waziri Mkuu anayepigwa vita Nuri al-Maliki wakati akigombania kubakia madarakani baada ya washirika wake wakuu wa zamani kuacha kumuunga mkono na wananchi wa Iraq wakizidi kuelezea mashaka yao juu ya uwezo wake wa kuiunganisha nchi hiyo. Hata hivyo al-Maliki hadi sasa hakuonyesha ishara yoyote ile hadharani ya kutaka kun'gatuka na badala yake amekuwa akijiandaa kwa kipindi cha tatu madarakani kama waziri mkuu baada ya kundi lake kujishindia wingi wa viti bungeni katika uchaguzi uliofanyika mwezi wa Aprili.
Marekani na mataifa mengine makubwa yamekuwa yakimshinikiza al -Maliki kuunda serikali yenye ushirikishi zaidi itakayoijumuisha jamii za Wasunni na Wakurdi kushughulikia matatizo yanayoikabili nchi hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni