WATU 48 WAUAWA SHAMBULIO LA KIGAIDI KENYA:
48 wauwawa katika shambulio Kenya
Takriban watu 48 wameuwawa wakati wanamgambo wanaotuhumiwa kuwa wa Al Shabab kutoka Somalia walipouvamia mji wa mwambao wa Kenya na kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya kituo cha polisi,hoteli na ofisi za serikali.
Magari yaliyoteketea nje ya kituo cha polisi cha Mpeketoni kufuatia shambulio la Jumapili. (15.06.2014)
Watu wenye silaha nzito waliingia kwa magari kwenye mji wa Mpeketoni karibu na kisiwa cha mwambao cha Lamu kilicho mashuhuri kwa watalii wakati wa usiku wa Jumapili.
Walioshuhudia tukio hilo wamesema kwanza walikishambulia kituo cha polisi kabla ya kuwafyatulia ovyo risasi raia baadhi yao walikuwa wakiangalia michuano ya soka Kombe la Dunia katika vilabu vya pombe na mahoteli.
Naibu mkuu wa wilaya Benson Maisori amesema majengo kadhaa katika mji huo ambao uko kama kilimota 100 kutoka mpaka na Somalia yametiwa moto yakiwemo mahoteli, mikahawa,mabenki na ofisi za serikali.
Washambuliaji wanafikia 50
Amekaririwa akisema "Kulikuwa na washambuliaji wanaofika hamsini,wakiwa na silaha nzito kwenye magari matatu na walikuwa na bendera ya Al Shabab.Walikuwa wakitowa mayowe kwa Kisomali na kutamka 'Allahu Akbar'(Mungu Mkubwa)"
Mkaazi mmoja wa mji huo aliyeshuhudia tukio hilo John Waweru mwenye umri wa miaka 28 amesema kaka zake wawili wameuwawa katika shambulio hilo.
Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba washambuliaji hao waliingia kama saa tatu usiku na amewasikia wakipiga mayowe kwa Kisomali huku wakifyetuwa ovyo risasi na kwamba kaka zake wawili wameuwawa na yeye aliweza kunusurika baada ya kukimbilia nyumbani na kujifungia.
Mapambano makali ya risasi yaliendelea hadi usiku wa manane lakini jua lilipokuchwa Jumatatu ya leo imeripotiwa kwamba hali ilikuwa shwari katika mji huo wa Mpeketoni ambapo vikosi vya usalama vinasema vinawasaka washambuliaji na kutafuta miili ya watu waliopoteza maisha yao.
Idadi kubwa ya maafa
Polisi mmoja katika mji huo amesema maiti 47 zimefikishwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti na Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya kimethibitisha kwamba watu 48 wameuwawa.
Afisa wa uhusiano wa chama hicho katika eneo hilo Wariko Waita amesema kuna watu waliojeruhiwa waliowapeleka hospitali katika mji huo na Lamu na kwamba wanaendelea kushirikiana na polisi kuwatafuta watu wengine ambao hawajulikani walipo.
Mkuu wa jeshi la polisi la Kenya David Kimaiyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba maafisa wao bado wanaendelea kulipekuwa eneo hilo na kwamba huo ni unyama ambao wasingependa kuona unarudiwa tena mahala popote pale.
Amesema "Tunashuku kuhusika kwa Al Shabab katika shambulio hili.Tunatowa wito wa utulivu wakati tukijitahidi kuwasaka washambuliaji.Ni kisa cha bahati mbaya sana."
Harakati za Al Shabab
Vikosi vya Kenya vilivuka mpaka na kuingia kusini mwa Somalia hapo mwaka 2011 kupambana na Al Shabab na baadae kujiunga na kikosi cha wanajeshi 22,000 wa Umoja wa Afrika kupambana na wanamgambo hao wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda.
Al Shabab liliapa kulipiza kisasi na kufanya mashambulizi kadhaa katika ardhi ya Kenya likiwemo shambulio la mwezi wa Septemba mwaka jana katika jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi ambapo takriban watu 67 waliuwawa.
Mji wa Mpeketoni ni kituo cha biashara kilioko kwenye barabara kuu ya mwambao uko kwenye eneo la bara kama kilomita 30 kusini magharibi mwa kisiwa cha Lamu ambacho ni mashuhuri kwa watalii na usanifu wake wa majengo ya kale umeorodheshwa kuwa eneo la Turathi ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO.
Maiti barabarani
Msemaji wa jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir ameelezea jinsi watu hao waliokuwa na bunduki walipouvamia mji huo na kuwazidi nguvu polisi wa eneo hilo na kuwafyatulia risasi watu walio mjini kutoka kwenye magari yao.
Chirchir pia amesema washambuliaji hao "yumkini wakawa ni Al Shabab" juu ya kwamba hakuna madai ya kuhusika na shambulio hilo yaliyotolewa mara moja na kundi hilo.
Ndege za uchunguzi za kijeshi zilianza kazi mara tu baada ya kuanza kwa shambulio hilo.
Washambuliaji walijaribu kukivamia kituo cha polisi ikiwemo lagha ya silaha lakini Maisori amesema maafisa walilihami jengo hilo la polisi na kuwatimuwa wanamgambo hao.
Wakaazi walioko katika vijiji karibu na mji huo pia wameripoti kwamba wapiganaji hao waliyashambulia makaazi yao wakati walipokuwa wakiondoka kufuatia mapigano katika mji wa Mpeketoni.
Mkaazi wa kijiji cha Kibaoni kilioko kama kilomita tano nje ya mji wa Mpeketoni Mohammed Hassan amesema kulikuwa na miili sita ya mwanaume na mtoto ikiwa nyumbani na miili mengine minne ikiwa barabarani.
Vitisho vya mashambulizi
Mwezi uliopita mmojawapo wa makamanda waandamizi wa Al Shabab Fuad Mohamed Khalaf alitowa tangazo la radio lenye kuwahimiza wapiganaji wao kuishambulia Kenya.
Maelfu ya watalii wa Kingereza pia walihamishwa mwezi uliopita katika kituo hicho cha utalii cha mwambao cha Lamu kilioko karibu na mji wa bandari wa Mombassa kufuatia angalizo jipya la mashambulizi ya kigaidi kutoka wizara ya mambo ya nje ya Uingereza.
Uingereza wiki hii ilitowa tahadhari kwa raia wake katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki ikiwemo Djibouti,Ethiopia, Kenya na Uganda ambazo zote zina wanajeshi wao nchini Somalia kwa kutaja tishio la mashambulizi kwenye hadhara za kuangalia michuano ya soka Kombe la Dunia.
Kundi la Al Shabab limedai kuhusika na mauaji ya mwezi uliopita ya wanajeshi wawili wa Kenya katika wilaya hiyo hiyo ilioshambuliwa Jumapili juu ya kwamba ilikuwa katika eneo lilioko kaskazini zaidi karibu kabisa na eneo la mpaka na Somalia.
Maoni
Chapisha Maoni