Mkutano wa London wa kukomesha ghasia za kingono wakamilika leo.
Mkutano wa kilele wa siku nne unaonuia kukomesha ghasia za kingono katika nchi zinazokumbwa na vita unakamilika hii leo mjini London kwa hotuba itakayotolewa na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry
Mkutano huo ulioanza Jumanne wiki hii umeandaliwa na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Uingereza William Hague na mcheza filamu mashuhuri ambaye pia ni mjumbe maalum wa umoja wa Mataifa Angelina Jolie,wakiwa na nia ya kuimarisha kampeni ya kutokomeza ghasia za kingono kama silaha katika vita.
Waathiriwa wa ghasia hizo za kingono hapo jana walikuwa na fursa ya kuelezea madhira waliyoyapitia.Mmoja wao ni mwanahabari wa Colombia Jineth Bedoya Lima ambaye alielezea jinsi alivyoshambuliwa alipokuwa ameitembelea jela moja kuripoti kuhusu biashara haramu ya silaha.
Lima aliyebakwa mara kadhaa na genge la wafungwa anasema ni vigumu mno kwa mwanamke kuzungumzia ubakaji na mateso ya kingono aliyoyapitia lakini ana matumaini kuwa mkutano huo wa London utakuwa muamko mpya utakaowapa waathiriwa nguvu za kukabiliana na yaliyowakumba.
Muongozo watolewa wa kukabiliana na ghasia
Azimio la kimataifa lililopitishwa hapo jana linatoa muongozo kwa wale walioko katika nafasi za kuchukua maamuzi katika maeneo ya vita jinsi ya kutambua kuwa ghasia za kingono ni uhalifu wa kimataifa na jinsi ya kuchunguza visa hivyo.
Mkutano huo ambao unahudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 100 pia umeangazia athari za ghasia za kingono kwa wanaume na vijana. William Hague na Angelina Jolie tayari wameizuru Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Bosnia kuhamasisha jamii kuhusu suala hilo
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anatarajiwa kuuhutubia mkutano huo kupitia mawasiliano ya video.
Pembezoni mwa mkutano huo,wawakilishi kutoka Nigeria, Chad, Cameroon, Niger na Benin walikutana hapo jana kujadili hatua ambazo zilifikiwa mwezi uliopita mjini Paris za kukabiliana na kundi la waasi la Boko Haram na shughuli ya kuwaokoa wasichana wa shule waliotekwa nyara na kundi hilo.
Utekaji nyara wa wasichana wa Nigeria waangaziwa
Nchi hizo zimetoa tamko la pamoja na kuutaja utekaji nyara huo wa wasichana wa shule zaidi ya mia mbili miezi miwili iliyopita kuwa mfano mbaya zaidi wa ghasia za kingono na kutilia mkazo azma yao ya kulitokomeza kundi hilo.
Wawakilishi hao wa Nigeria na majirani zake waliungana na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya,Marekani, Umoja wa Afrika, Ufaransa,Canada,Uingereza na Umoja wa Ulaya kama ishara ya kuonyesha umoja katika kushughulikia kitisho cha Boko Haram.
Hague ameahidi Uingereza itatoa msaada zaidi wa mafunzo ya kiufundi kwa jeshi la Nigeria katika juhudi hizo za kuwatafuta wasichana hao na kutangaza kuwa Marekani imeanzisha mpango wa kuhakikisha wasichana milioni moja kutoka kaskazini mwa Nigeria ambako ni ngome ya Boko Haram wanapata elimu.
Wakati huo huo waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani Gerd Müller aliyekamilisha ziara ya siku tatu nchini Nigeria hapo jana aliahidi kiasi cha euro milioni mbili kwa ajili ya mfuko wa kimataifa ulioanzishwa kusaidia kuimarisha ulinzi katika shule nchini Nigeria.
Maoni
Chapisha Maoni