Poroshenko aahidi kutoiachia Crimea
Rais mpya wa Ukraine Petro Poroshenko Jumamosi (07.06.2014) ameapa kudumisha mamlaka ya dola ya nchi yake likiwemo jimbo la Crimea na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu na Umoja wa Ulaya.
Baada ya kula kiapo cha kuwa rais wa nchi hiyo mbele ya wageni wa heshima kutoka takriban nchi hamsini, Poroshenko ameapa katika hotuba yake hiyo ya kuapishwa kushika wadhifa huo "kutunza na kuimarisha umoja wa Ukraine" wakati akijiandaa kukabiliana na changamoto zinazotokana na vuguvugu la waasi mashariki mwa nchi hiyo.
Amesema "Sitaki vita. Sitaki kulipiza kisasi.Nataka amani na nitachukuwa hatua za kuhakikisha umoja."
Ametowa wito kwa wanaharakati wanaotaka kujitenga ambao wameikalia miji kadhaa mashariki mwa nchi hiyo katika uasi ambao mara nyengine ulisababisha umwagaji damu na makundi ya watu wenye silaha yenye kuipinga serikali wasalimishe silaha zao na kuahidi msamaha kwa wale ambao hawana damu mikononi mwao.
Katika hotuba yake hiyo aliyoitowa bungeni mjini Kiev Poroshenko amewaahidi wakaazi wa eneo la mashariki la Donbass ambalo kwa sehemu kubwa liko mikononi mwa waasi kwamba atatowa mamlaka zaidi mikoani na kuhakikisha matumizi ya lugha ya Kirusi bila ya kikwazo.
Crimea ni sehemu ya Ukraine
Pia amesema hakutakuwa na muafaka katika suala la hatima ya Rasi ya Crimea ambayo imenyakuliwa na Urusi hapo mwezi wa Machi baada ya kura ya maoni yenye utata kuonyesha kwamba takriban wakaazi wake wote wanapendelea kujitowa Ukraine.
Katika hotuba yake iliokuwa ikishangiliwa amesema wananchi wa Ukraine katu hawatoweza kufurahia uzuri wa amani venginevyo wanautuliza uhusiano wao na Urusi na kusisitiza kwamba "Crimea ilikuwa na itaendelea kuwa ardhi ya Ukraine".
Ameongeza kusema ameufikisha ujumbe huo kwa ufasaha kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi wakati viongozi hao walipokutana Ijumaa nchini Ufaransa kwa maadhimisho ya miaka sabini ya "D-Day".
Uhusiano na Umoja Ulaya
Poroshenko amesema anakusudia kusaini mkataba wa kiuchumi ambao ni sehemu ya Makubaliano ya Ushirikiano na Umoja wa Ulaya kwa kusema kwamba hiyo ni hatua kuelekea kwenye uwanachama kamili wa umoja huo.
Mtangulizi wake Viktor Yanukovych aliondolewa madarakani hapo mwezi wa Februari kufuatia ghasia za barabarani zilizozuka kutokana na kukataa kwake kujiunga na Makubaliano ya Ushirikiano na Umoja wa Ulaya na badala yake kupendelea uhusiano wa karibu zaidi na Urusi.
Wazo la kuwa na ushirkiano na Umoja wa Ulaya lilikuwa likuchukiwa na Urusi ambayo ilikuwa inataka kuendelea kuiweka Ukraine chini ya kivuli cha ushawishi wake baada ya enzi ya mmungano wa Kisovieti.
Poroshenko rais wa tano wa Ukraine tokea nchi hiyo ijipatie uhuru wake alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa tarehe 25 mwezi wa Mei baada ya kuahidi kuwaunganisha wananchi wa nchi hiyo walioko magharibi na mashariki jambo ambalo limeigawa nchi hiyo na kuitumbukiza katika vita vya kujinusuru.
Matarajio kukomeshwa machafuko
Waukraine wanataraji kuchaguliwa kwa Poroshenko mwenye umri wa miaka 48 ambaye ameowa na ana watoto wanne atafanikiwa kukomesha kipindi cha machafuko mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo ya baada ya enzi ya muungano wa Kosovieti.
Zaidi ya watu 100 wameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi mjini Kiev katika maandamano ya mitaani ambayo hatimae yalimuangusha Yanukovych na upande wa mashariki watu kadhaa wakiwemo wapiganaji wanaotaka kujitenga na wanajeshi wa serikali wameuwawa katika mapigano tokea mwezi wa Aprili.
Uasi wa mashariki sio changamoto pekee inayomkabili Poroshenko ambaye inairithi nchi ikiwa kwenye ukingo wa kufilisika,bado ikitegemea Urusi kwa gesi ya asili na kutajwa kuwa mojawapo ya nchi zilizotopea rushwa kubwa na yenye utawala mbaya kabisa barani Ulaya.
Kanda ya vita
Tokea kuchaguliwa kwa Poroshenko vikosi vya serikali vimeimarisha operesheni zake dhidi ya waasi wanaotaka kujitenga mashariki ya Ukraine ambao wanataka kujienguwa kutoka nchi hiyo na kuwa sehemu ya Urusi. Waasi wamejibu mashambulizi hayo na kuzigeuza baadhi ya sehemu hizo za mashariki zenye wakaazi wengi wanaozungumza Kirusi kuwa kanda ya vita.
Hapo Ijumaa walidungua ndege ya kijeshi ya Ukraine na kumuuwa mwanajeshi wa kikosi maalum cha wizara ya mambo ya ndani katika ngome kuu ya waasi huko Saviansk. Poroshenko ameapa hatokubali kuachilia kuwepo magari yaliosheheni "majambazi" na kuwahimiza waasi wanaoiunga mkono Urusi kusalimisha silaha zao pamoja na kuwahakikishia wapiganaji wa Urusi njia ya salama kurudi kwao.
Pia ametowa ujumbe wa kuwatuliza wakaazi hao wa mashariki na kuzungumza nao kwa Kirusi badala ya lugha ya Ukraine ambapo amewaambia kuwa wamelaghaiwa kuhusu hekaya za viongozi wa serikali ya Kiev zilizochochewa na propaganda za Urusi na ukoo wa Yanukovych ambaye amemshutumu kwa kugharamia ugaidi.
Mapigano kusitishwa
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kulia), Rais Petro Poroshenko wa Ukraine(katikati) na Rais Vladimir Putin wa Urusi wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya "D-Day" Benouville,Ufaransa. (06.06.2014)
Hivi karibuni Poroshenko alikutana na Rais Barack Obama wa Marekani ambaye aliukaribisha vyema uongozi wake na pia amekutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Katika mkutano mfupi nchini Ufaransa hapo Ijumaa ambapo walikuwa wakihudhuria maadhimisho ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia maafisa wa Ufaransa wamesema Poroshenko na Putin walipeana mikono na kukubaliana kwamba mazungumzo ya kina kuhusu usitishaji wa mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi yataanza hivi karibuni.
Putin amewaambia waandishi wa habari anayakaribisha mapendekezo yaliyotolewa na Poroshenko kwa ajili ya kuumaliza mzozo huo.Hata hivyo amekataa kuyataja mapendekezo hayo na kusema kwamba Ukraine lazima isitishe kile alichokiita operesheni za kijeshi za "adhabu" dhidi ya wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi.
Sherehe za kuapishwa kwa Poroshenko katika bunge la Ukraine mjini Kiev hapo Jumamosi zimehudhuriwa na Rais Joachim Gauck wa Ujerumani,Bronislaw Komorowski wa Poland na Dalia Grybauskaite wa Lithuania. Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy walikuwa pia miongoni mwa wageni waalikwa waliohudhuria halikadhalika Rais Alexander Lushenko wa nchi jirani ya Belarus anayetajwa kuwa ni dikteta na rafiki wa karibu wa serikali ya Urusi.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP/AFP
Mhariri : Amina Abubakar
Maoni
Chapisha Maoni