MGONJWA AAMBUKIZWA ZIKA KUPITIA NGONO MAREKANI:


Maafisa wa afya nchini Marekani wanasema mgonjwa katika jimbo la Texas ameambukizwa virusi vya Zika kupitia ngono Na sasa watalaamu wamo mbioni kutengeneza chanjo ya kupambana na virusi hivyo.
Maafisa katika jimbo hilo wamesema virusi hivyo vimeambukizwa kupitia mgonjwa ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Venezuela. Zachary Thompson ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya mjini Dallas "Tuliangalia jinsi alivyowauma watu Amerika ya Kusini ambao wamesafiri kuingia Marekani, na kisha jinsi wanavyouma na kuambukiza virusi hivyo. Sasa tunazungumza kuhusu kuambukizwa virusi hivyo kupitia ngono. Inazusha wasiwasi kwa sababu ya watu ambao wanasafiri kwenda mataifa ya Amerika ya Kusini, na kushiriki ndono bila kinga, wanaoweza kuleta virusi hivi nyumbani na kuwaambukiza wengine"
Virusi vya Zika kwa kawaida husambazwa kupitia mbu anapomuuma binadamu. Lakini wachunguzi wamekuwa wakiangalia uwezekano kwamba virusi hivyo pia vinaweza kusambaa kupitia ngono.
Kuna kitisho kikubwa katika uhusiano kati ya virusi hivyo na matatizo ya watoto kuzaliwa wakiwa na ulemavu. Virusi hivyo vimepatikana zaidi katika mataifa ya Amerika kusini ambako watoto wengi wameripotiwa kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo kuliko kawaida.
Brasilien Zika Virus - Mikrozephalie Zika inahusishwa na watoto kuzaliwa na ulemavu
Kuna ripoti ya mtalaamu mmoja wa Colorado aliyepata virusi hivyo barani Afrika na kisha akamwambukiza mkewe nyumbani mwaka 2008, na pia vikapatikana katika mbegu za kiume za mwanamme mmoja katika kisiwa cha Tahiti.
Shirika la Afya ulimwenguni siku ya Jumatatu lilitangaza hali ya hatari duniani kote kuhusiana na kusambaa kwa virusi vya Zika, likisema ni “tukio lisilo la kawaida” ambalo linaweka kitisho kikubwa kwa ulimwengu mzima.
Kufikia sasa hakuna ushahidi kuwa Zika inaweza kusababisha kifo, lakini baadhi ya matukio yameripotiwa ambapo wagonjwa wamekuwa na matatizo makubwa.
Watu wanaougua ugonjwa wa Zika kawaida hujiskia kuwa na homa, upele, maumivu ya misuli na viungo na uchovu dalili ambazo zinaweza kudumu kwa siku mbili hadi saba. Lakini karibu asilimia 80 ya watu walioambukizwa huwa hawapati dalili hizo. Dalili za ugonjwa huo ni sawa na zile za homa ya dengue ambayo husababishwa na mbu sawa na anayeambukiza Zika.
Ni vipi ugonjwa wa Zika unavyoweza kudhibitiwa?
Juhudi za kudhibiti usambaaji wa virusi zinaangazia zaidi katika kuyaangamiza maeneo ya kuzaana mbu na kuchukua tahadhari dhidi ya kuumwa na mbu kama vile kutumia dawa za kuuwa mbu na vyandarua vya kuzuia mbu.
Maafisa wa Afya wamesema visa vya Zika vimeripotiwa katika zaidi ya nchi 30 kuanzia mabara ya Amerika hadi Ireland na Australia. Brazil ndio nchi iliyoathirika kwa kiasi kikubwa.
Miripuko wa ugonjwa wa virusi vya Zika awali iliripotiwa barani Afrika, Amerika, Kusini mwa Asia na Pasifik Magharibi. Virusi hivyo viligundulika kwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka wa 1947 katika aina Fulani ya tmbili na ikatambuliwa katika watu mwaka wa 1952 nchini Uganda na Tanzania kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Nani aligharamia ukarabati wa kifahari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA