BREAKING NEWZZ.....Ofisi za CCM Kengeja Pemba zachomwa moto
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vikali kitendo cha kuwekwa alama ya X nyumba kadhaa za wafuasi wake Kisiwani Pemba hivi karibuni.
Aidha, kimesikitishwa na kulaani vikali kitendo cha kuchoma moto Tawi la CCM la Kengeja, kilichofanywa na watu wasiojulikana usiku wa kumkia leo.
Hayo yamesema na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bibi Waride Bakari Jabu, alipokuwa akizungumza na Wanahabari hapo Afisini kwake Kisiwandui, Mjini Unguja.
Amesema kitendo cha kuweka alama ya X kwenye nyumba za wafuasi wa CCM pekee katika maeneo ya Mtambile, Kengeja, Minazini na Kangani Wilayani Mkoani sio tu kina lengo la kuvunja amani iliyopo nchi bali pia kinakwenda kinyume na sheria na taratibu za Taifa letu.
“Kwa niaba ya CCM nachukua nafasi hii kulaani vikali na kuwataka wale wote waliohusika na vitendo hivyo, waache mara moja, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria na taratibu za nchi yetu” na kuongeza kusema kuwa kinapaswa kulaaniwa na kila mpenda amani na ustawi wa demokrasia ya kweli nchini”. Alidai Bi. Waride.
Ametoa wito kwa Wazanzibari hasa wafuasi wa CCM kupuuza vitendo hivyo, na badala yake waelekeze nguvu zaidi katika maandalizi ya uchaguzi wa marudio uliotangazwa kufanyika Machi 20, ili kukiletea ushindi wa kishindo Chama hicho (CCM).
Kuhusu kuchomwa moto Tawi la CCM Kengeja, Bibi Waride amesema Chama Cha Mapinduzi kimeshtushwa na kitendo hicho, kwani sio tu kinarejesha nyuma maendeleo ya chama, bali pia kinawatia hofu wana CCM wa maeneo husika.
Amesisitiza haja kwa Vyombo vya Ulinzi hasa Jeshi la Polisi kuwatafuta wale wote waliohusika na hujuma hiyo, na kuwafikisha mbele ya Vyombo vya Dola ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Maoni
Chapisha Maoni