BREAKING NEEEWS! Takribani wahamiaji 700 wahofiwa kuzama.
Muda mchache baada ya taarifa za kuzamishwa kwa boti iliyobeba zaidi ya wakimbizi 700 kwenye bahari ya Mediterania kuibuka, boti nyengine mbili zimezama Libya na kusababisha vifo vya watu 70.
Moja ya boti zilizowabeba wahamiaji haramu kutoka Afrika kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterenia.
Msemaji wa kikosi cha ulinzi wa pwani cha Libya, Qaasim Ayoub, ameliambia shirika la habari la AP kwamba waokoaji wanaendelea kuopoa miili inayosukumwa na mawimbi umbali wa kilomita 18 kutokea wilaya ya Tajoura mjini Tripoli. Aliongeza kwamba wahamiaji 36 wa Kiafrika, wakiwemo wanawake watatu - mmoja wao akiwa mjamzito wameokolewa.
Kamanda wa kikosi cha Walinzi wa Pwani cha Libya, Ali Sarti, amesema boti za doria zimewaokoa wahamiaji waliokuwa kwenye boti iliyokwishavunjika katikati ya bahari
"Vikosi vyetu vya doria vilikuwa baharini jana na kugundua boti iliyovunjika na kuharibika katikati ya bahari. Kulikuwa na wahamiaji wamelala kwenye boti hiyo baada ya kuzama na waliokolewa. Waliookolewa ni watu 36 miongoni mwa wahamiaji 97, kwa mujibu wa wahamiaji wengine, wakiwamo wanawake na watoto," alisema Sarti.
Miongoni mwa waliookolewa ni kijana mmoja wa kiume, ambaye licha ya kuwa na sura ya Kiafrika, anazungumza Kiarabu fasaha, na hivyo kuzua wasiwasi ikiwa kweli wahamiaji hao ni wale wanaootokea kusini mwa jangwa la Sahara pekee, au hata nchi za Kiarabu kaskazini mwa Afrika.
"Kulikuwa na matatizo kwenye boti, mulikuwa na watu 105, 36 tu ndio waliopona na 70 wamekufa. Kisha boti ya polisi ikaja kutoka baharini na kuwaokoa watu 36, wanawake watatu na mtoto mmoja walikufa," alisejma kijana huyo.
Watu 700 wahofiwa kufa maji
Taarifa ya maafa haya inakuja muda mchache baada ya kuibuka kwa habari za ajali nyengine mbaya kabisa kuwahi kutokea katika siku za karibuni, ambapo wahamiaji wanaokisiwa kufikia 700 wamekufa maji.
Shirika la Wahamiaji Duniani (IOM) limesema ikiwa ripoti zinazotolewa na manusura wa ajali hiyo iliyotokea Jumatano iliyopita karibu na Malta, zitakuwa za kweli, basi mkasa huu hautachukuliwa kama ajali, bali mauaji ya maangamizi yanayofanywa na wahalifu wanaoratibu safari hizo za hatari kwa wakimbizi wanaotaka kuingia barani Ulaya kwa njia ya bahari.
Manusura wawili wa Kipalestina ambao waliokolewa siku ya Alhamisi, wameliambia shirika hilo la wahamiaji kwamba kiasi cha abiria 500 walikuwa kwenye chombo kimoja ambacho kiliharibiwa kwa makusudi na wasafirishaji haramu.
Kwa mujibu wa manusura hao, wahamiaji kutoka Syria, Palestina, Misri na Sudan waling'oa nanga kutoka mji wa Damietta, Misri, tarehe 6 mwezi huu, na kulazimishwa kubadilisha boti mara kadhaa wakati wa safari yao kuelekea Ulaya.
Wasafirishaji hao haramu ambao walikuwa kwenye boti nyengine, waliwaamuru kuingia kwenye boti ndogo zaidi lakini walikataa kwa kuwa walihofia kuzama, na hapo ndipo wasafirishaji walipoitoboa boti kubwa waliyokuwamo hadi ilipozama.
Maoni
Chapisha Maoni