ZITTO AMWAGA MACHOZI UKUMBINI
Mpango mzima ulioshuhudiwa na paparazi wetu ulijiri kwenye Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni jijini Dar ambapo Bendi ya Malaika, chini ya Christian Bella ilikuwa ikishusha burudani ya kufa mtu.
Wakati Mbunge wa Jimbo la Sikonge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Said Nkumba alitesa kwenye jukwaa la Msondo Ngoma pale TTC Chang’ombe, Temeke, Zitto alifunika vibaya Mango Garden, Kinondoni, kwani alikuwa zaidi ya shabiki, pedeshee na mwimbaji.
Katika muda ambao watoto wa mjini husema ni usiku mnene, Zitto ambaye yupo katika mgogoro na chama chake, alipanda jukwaani wakati prezidaa wa Malaika Band, Christian Bella ‘Obama’ akiimba wimbo wake mpya wa ‘Nani Kama Mama’ ambapo mheshimiwa huyo alichotwa na hisia za kibao hicho hadi kujikuta akimwaga machozi kwa kumbukumbu ya msiba wa mama yake mzazi uliotokea mwaka jana (Shida Salum, alifariki Juni 1, 2014 jijini Dar es Salaam).
Mh. Zitto Kabwe akiteta jambo na wanamuziki wa Bendi ya Malaika.
“Lilikuwa ni tukio la kushangaza kwa mheshimiwa, maana alipanda
stejini kisha akajiunga na waimbaji, akachukua gitaa na kuanza kucharaza
kana kwamba alifanya nao mazoezi,” alisema shabiki mmoja ukumbini hapo,Hata hivyo, baadaye mwanasiasa huyo kijana kipenzi cha wengi, aliimarika na kuendelea kuuimba wimbo huo huku akiserebuka kwa kwenda mbele.
Baada ya kuona hivyo, mashabiki walimiminika jukwaani kupiga naye picha kwa muda wa takriban dakika 20, ambapo mbunge huyo alithibitisha kuwa ni mtu wa watu kwani shughuli zote zilisimama kwa muda ukumbini humo.
Katika hali hiyo, mapedeshee, ambao hung’ara katika kumbi kwa kutunza waimbaji na wanenguaji, walizimwa ngebe zao kwani Zitto alifunika kwa kutoa ‘mshiko’ wa kufa mtu.
Ilifahamika kwamba, Bella peke yake alipokea zaidi ya noti 50 za elfu kumi-kumi za Kitanzania kutoka kwa Zitto huku nyingine zikiwa ni dola za Kimarekani.
Wakipiga picha ya pamoja.
Hata hivyo, katika hali nyingine, baadhi ya watu walihoji usalama wa
Zitto kuwa ni sawa na sifuri katika kipindi hiki ambacho bado sakata la
kashfa ya uchotwaji wa mabilioni kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta
linaendelea kushika kasi na vigogo kufikishwa mahakamani.Watu hao walisema kwa namna Zitto alivyoingia ukumbini hapo na kujichanganya na mashabiki, ni rahisi kwa mtu mwenye nia mbaya kuweza kumdhuru, hasa watu wa Escrow ambao wana mapesa yanayoweza kuwashawishi kumfanya lolote.
“Watu wanatetemeshwa na hili skendo, leo wakimuona Zitto hapa kajiachia namna hii, watakumbuka jinsi alivyosimama kidete bungeni kutaka waliohusika wawajibishwe na fedha zirudishwe, unadhani nani hajui utamu wa fedha,” alisikika shabiki mmoja akisema.
Zitto alitafutwa kupitia simu yake ya mkononi ili kupata maoni yake juu ya usalama wake, lakini iliita bila kupokelewa.
Maoni
Chapisha Maoni