PANYA ROAD 510 WATIWA MBARONI!


Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova 


Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imewakamata vijana 510 wanaodaiwa kuhusika na mtandao wa uhalifu maarufu ‘Panya Road’ katika wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala.
Mbali na hilo, wazazi na walezi wa watuhumiwa hao wameonywa kutokwenda katika vituo walivyohifadhiwa vijana wao hadi polisi itakapojiridhisha baada ya upelelezi.
Januari 2, maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yalikumbwa na taharuki kubwa kwa saa mbili baada ya kuwapo kwa uvumi wa kundi hilo kuvamia mitaa mbalimbali na kupora mali.
Baada ya tukio hilo, polisi waliendesha msako mkali na kuwakama vijana 36 wenye rekodi ya kufanya uhalifu.
Jana, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema watuhumiwa wengine 510 walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya vijiweni na wengine wakifuatwa katika nyumba wanazoishi baada ya polisi kupata taarifa za kiintelijensia.
“Kati ya hao 510, kuna viongozi wao wakubwa watatu ambao ndiyo vinara wa kuhamasisha wenzao kufanya uhalifu. Kila msiba wa mwanachama mwenzao unapotokea ukiwamo ule wa juzi wa Magomeni, Kagera viongozi hao hawakosi kuhudhuria,” alisema Kova na kuongeza:
“Tulipowapekua watuhumiwa hawa tuliwakuta na vichocheo kadhaa vya uhalifu ambavyo ni puli za bangi 113, kete zake 676 na misokoto 294 na vinginevyo.”
Kova aliwataka wazazi na wa watuhumiwa hao kutojisumbua kwenda katika vituo vya polisi walikohifadhiwa... “Sasa hivi ni moja kwa moja mahakamani ili sheria ikichuke nafasi yake maana tumekuwa tukilalamikiwa polisi tukiwaachia watuhumiwa hawa kiholela sasa hakuna dhamana,” alisisitiza Kova.
Alisema operesheni ya kupambana na ‘Panya Road’ itakuwa endelevu hadi pale jina hilo ambalo limekuwa gumzo litakapotoka masikioni mwa watu.
Alisema polisi wamejipanga kutoa mafunzo maalumu kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa mikoa yote ya kipolisi Dar es Salaam ili kukabiliana na vitendo hivyo vya uhalifu.
“Ni ukweli usiopingika kuwa vijana wanaofanya vitendo hivi wanafahamika kwa wananchi wa eneo husika lakini wanakuwa wasiri kufichua uovu huo. Mafunzo haya yatasaidia kuondoa tatizo hili,” alisema Kova.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Nani aligharamia ukarabati wa kifahari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA