Miss Tanzania Mpya 2014 Lilian Kamazima Yadaiwa Ni Mnyarwanda, Apondwa Kuwa Ni Mbaya.
Lilian Kamazima |
Mwenzako akinyolewa
wewe tia maji !......Zengwe jipya limeibuliwa jana na kuenezwa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba Lilian Kamazima aliyepewa taji hilo baada ya
Sitti Mtemvu ambaye ni mshindi wa awali kujivua taji kutokana tuhuma za
kudanganya umri, si raia wa Tanzania bali ni Mnyarwanda.
Hayo yameibuka siku mbili tangu Lilian kukabidhiwa taji la Miss Tanzania
2014, lililokuwa likishikiliwa na Sitti Mtemvu aliyeamua kulivua baada
ya kukumbwa na kashfa mbalimbali tangu kutawazwa kwake Oktoba 11.
Ukiachilia mbali hilo la uraia tangu apewe taji hilo juzi kwenye
mitandao ya kijamii mashabiki wa urembo wamekuwa wakimponda Lilian kuwa
ni mbaya sio mzuri wa kuwa Miss Tanzania.
Lilian ambaye awali alikamata nafasi ya pili kwa mujibu wa Mwanaspoti
alisema: “Sikuwa na kinyongo ukizingatia urembo ni mambo mengi si sura,
ngozi, mwonekano pekee bali unajumuisha mambo mengi, ndiyo maana
kipindi cha usahili huwa kirefu. Binafsi niliamini kwamba (Sitti)
alistahili hasa kutokana na kuwa na vigezo vingi vinavyoonekana kwa
macho hata tulipokuwa kambini, nilikubali matokeo,”
Lilian alisema kipindi cha mwezi mmoja tangu kutolewa kwa matokeo Oktoba
11, anaamini kilikuwa kigumu kwa Sitti, pia kwake hasa ukizingatia
tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili mrembo huyo aliyetokea katika
Kanda ya Temeke.
“Nina maono ya mbali na ninatamani miaka mitano ijayo niione Tanzania
iliyokua hasa katika nyanja ya elimu, napenda kuona namba ya wanafunzi
wanaofaulu ikiwa sawa vijijini na mijini ili kuwa na taifa lenye watu
werevu na wenye maendeleo, hivyo nitajitahidi kutumia nafasi yangu
kusongesha gurudumu hili,” alisema.
Mrembo huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Uganda kwa shughuli za masuala
ya mitindo, alisema anafurahia kupata nafasi hiyo na anawaahidi
Watanzania kuwa atafanya kazi kwa nguvu zote ili kuhakikisha anatimiza
malengo ya waandaaji wa mashindano hayo. Lilian Kamazima ana miaka 18,
alishiriki akitokea Mkoa wa Arusha.
Maoni
Chapisha Maoni