CHEKI VURUGU YA JANA KUMNUSURU WARIOBA!

 

Kabla ya Jaji Warioba kuanza kuzungumza katika mdahalo huo ambao pia ulihudhuriwa na makada wa CCM na Chadema, Butiku alisema: “Hayawi hawayi, sasa yamekuwa. Tume imeshamiliza kazi na Bunge nalo lmeshamaliza kazi yake. Lengo ni moja tu, ni maendeleo yetu sote.”

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba jana alivamiwa na kikundi cha watu wachache waliohudhuria mdahalo wa Katiba wakati akihoji vitendo vya baadhi ya watu kutumia vibaya jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.Jaji Warioba, ambaye alikuwa msemaji mkuu kwenye mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alikuwa akihitimisha hotuba yake aliyoianza saa 9:15 alasiri, kwa kuhoji kuhusu watu wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Nyerere kupitisha hoja zao katika misingi isiyokubalika.Vurugu hizo zilidumu kwa takriban dakika 45 ndani ya ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Blue Pearl, Ubungo lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida wasaidizi wa waziri huyo mkuu wa zamani, walimtoa ukumbini dakika 30 baada ya sakata hilo kuanza, hali iliyowapa nafasi vijana hao walionekana kujiandaa kufanya vurugu, kumsogelea na kumpiga. Baadhi ya watu walionekana kumzonga Jaji Warioba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni pamoja na aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Paul Makonda. Baada ya tukio hilo, polisi waliokuwa na silaha na wakiwa wamevalia nguo za kiraia walimtoa Jaji Warioba ukumbini.Makonda na Amon Mpanju, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, nao waliokolewa na polisi kutokana na vijana walioonekana kumuunga mkono Jaji Warioba kuwatuhumu kuhusika kwenye vurugu. Makonda aliambulia kipigo na kulazimika kujificha katika moja ya ofisi zilizopo hotelini hapo.
Mbali na Jaji Warioba, wajumbe wenzake wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambao ni Humphrey Polepole, Profesa Paramagamba Kabudi, Profesa Mwesiga Baregu, Awadhi Said na Ester Mkuchu nao walitolewa kwenye ukumbi huo na kupelekwa katika chumba maalum hotelini hapo.
Akitolea mfano watu wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Nyerere kiasi cha kuwashangaza hata wale waliowahi kuishi naye kwa karibu, Jaji Warioba alihoji iwapo Mwalimu Nyerere angekuwa hai angekubali mambo haya yapite.
Baadhi ya mambo aliyodai kuwa hata Mwalimu Nyerere asingeweza kuyapinga ni miiko ya uongozi, viongozi kupokea zawadi na kuzimiliki.
“Watu walimuandikia barua Mwalimu Nyerere kumshawishi kuwa fedha zake zitakuwa salama kama ataziweka nje ya nchi, siyo kama alikataa tu, alitangaza jambo hilo katika vyombo vya habari,” alisema.
Huku akizungumza kwa mtindo wa kuuliza swali Jaji Warioba alisema: “Nauliza, hivi, Mwalimu Nyerere angekataa miiko ya uongozi isiingizwe katika katiba? Angekubali watu wawe na akaunti nje ya nchi? Watu wapate zawadi wakae nazo? Labda huyo si Mwalimu.”
Jaji Warioba, ambaye alianza kushangiliwa kwa nguvu baada ya kuzungumza mambo hayo, alisema: “Kwa sisi tunaomjua vizuri Mwalimu, tunajua kuwa ndio yuleyule ambaye alilipitia Azimio la Arusha lililokuwa msingi wa utu na kutoona hata sehemu moja yenye makosa ya kurekebisha.”
Mifano hiyo iligeuka ‘mwiba mchungu’ kwa baadhi ya waliohudhuria mdahalo huo ambao walionekana kujiandaa kutokana na kwenda ukumbini hapo na mabango yanayoonyesha kukubali Katiba Inayopendekezwa.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Nani aligharamia ukarabati wa kifahari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA