DARAJA LA KIGAMBONI KUANZA KUTUMIKA MACHI MOSI
……………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano sehemu ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amesema
daraja la Kigamboni litaanza kutumika kuanzia Machi mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukagua
hatua za ujenzi wa daraja hilo Eng. Nyamhanga amemtaka msimamizi wa
ujenzi huo kuhakikisha hatua ya ujenzi iliyobaki inakamilika katikati ya
mwezi februari na kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi Machi.
“Hakikisheni Machi mosi magari
yaanze kupita rasmi kwenye daraja hili na hivyo kufungua ukurasa mpya
kwa wakazi wa Kigamboni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na
msongamano katika eneo la Magogoni”, amesema Eng. Nyamhanga.
Eng. Nyamhanga amesisitiza kuwa
Serikali inaangalia uwezekano wa kuunganisha daraja la Kigamboni na
barabara ya Charambe,Mlandizi hadi Chalinze ili kupunguza msongamano wa
magari katikati ya Jiji.
Amemtaka meneja wa mradi wa ujenzi
wa daraja hilo toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. John Msemo
kuhakikisha anatafuta Wakala makini atakayesimamia na kuendesha mradi
huo.
Daraja la Kigamboni lenye urefu wa
mita 680, unasimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS) na Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano
linatarajiwa kuishi zaidi ya miaka 100 na kuwa na uwezo wa kupitisha
mizigo ya tani 56 zinazokubalika katika nchi za jumuiya ya madola.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
Maoni
Chapisha Maoni