MAWAZIRI WATATU WA RAIS MAGUFULI WAZUA UTATA ,MENGI YASEMWA,
Na ibara ya 55 (4) inamuelekeza Rais kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge.
Kwa
kutumia mamlaka hayo, Alhamisi iliyopita Rais Magufuli aliwateua makada
watatu kuwa wabunge na hapo hapo kutangaza kuwateua kuwa mawaziri na
kisha kuwaapisha juzi kutumikia wadhifa huo.
Mawaziri
hao ni Profesa Makame Mbarawa ambaye ameteuliwa kuwa Wazira wa Maji na
Umwagiliaji, Dk Abdallah Possi (Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), na Balozi Augustine Mahiga
ambaye anakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Kuteuliwa
kwao kunafanya jumla ya wabunge walioteuliwa na Rais hadi sasa kuwa
wanne baada ya kumteua Dk Tulia Ackson mwezi uliopita kabla ya naibu
mwanasheria mkuu huyo wa zamani kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge.
Hata
hivyo, Dk Tulia aliapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kabla ya
kugombea nafasi ya unaibu spika na kushinda na kuapishwa kabla ya kuanza
kutekeleza majukumu yake.
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema
hapo kuna tatizo la kisheria kwa kuwa mawaziri wote huteuliwa kutokana
na nafasi zao za ubunge na kwamba kiapo cha ubunge ndiyo kinamtambulisha
mbunge kabla ya kutambuliwa kuwa waziri.
Lissu
alisema endapo shughuli za Kamati za Bunge za Kudumu zitaanza vikao
vyake siku chache zijazo kabla ya mkutano wa Bunge, waziri anayehusika
kwenye kamati yake hatatambuliwa licha ya kuwa kiongozi wa Serikali
anayetakiwa kujibu hoja za wizara yake.
“Kwa
mfano, Balozi Mahiga atahitajika kuwa mjumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje,
sasa ataingiaje bila kuwa na kiapo cha kuwa mbunge? Je, hawataenda
kushiriki? Kama hawataenda, itakuwaje kwa sababu hata kanuni zinasema
huwezi kutambuliwa wala kufanya kazi za kibunge bila kula kiapo,”
alisema Lissu.
Kauli
ya Lissu iliungwa mkono na mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Amir Manento kuwa waziri
aliyeapishwa bila kula kiapo cha Bunge hawezi kutambuliwa na Bunge hilo.
Jaji
Manento alisema Spika hatakuwa na uwezo wa kumpangia kazi zozote za
kibunge hadi atakapokula kiapo. Kwa hiyo alisema mawaziri walioapishwa
kabla ya kiapo hicho hawatambuliwi na Bunge.
“Inawezekana
Rais alishawateua mapema katika kipindi cha ukimya wake wa mwezi mmoja
na kuwasiliana na ofisi za Bunge, bila kupata taarifa hiyo, yaani ofisi
ya Bunge ikawatambua tu licha ya kutotambuliwa kwa kiapo, lakini bado
kuna utata katika suala hilo la kiapo, sawa na mchezo wa yai na
kifaranga nani aliyeanza,” alisema Jaji Manento.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mawaziri hao hawawezi kujihusisha na shughuli zozote za Bunge bila kula kiapo.
Alisema
mawaziri hao watakuwa na nafasi ya kufanya shughuli zote zinazowahusu
kama mawaziri, lakini hawatakuwa na nafasi ya kupewa majukumu ya kibunge
kabla ya kula kiapo.
“Jambo
la pili, mawaziri hao wanaweza kuwa na nafasi ya kushiriki kwenye
Kamati za Bunge lakini hawatakuwa na nafasi ya kupiga kura kama kanuni
za Bunge zinavyobainisha. Anaweza kuingia na kusikiliza au kufuatilia
mjadala tu kwenye kamati hizo,” alisema huku akitoa mfano kuwa jambo
hilo si mara ya kwanza kutokea.
“Profesa
(Sospeter) Muhongo aliteuliwa kuwa mbunge na kuapishwa waziri wakati
Kamati za Bunge zikianza vikao vyake, lakini hakuwa ameapa kuwa mbunge
kwa hivyo aliingia na kufuatilia vikao, lakini hakuwa na haki ya kupiga
kura.”
Katika
ufafanuzi huo, Dk Kashililah alisema mawaziri hao hawataweza kushiriki
mjadala ya miswada au hoja zilizowasilishwa ndani ya kamati hizo.
“Na ndiyo maana Bunge litakapoanza tu, wanaanza kula kiapo kwanza kwa sababu kanuni za Bunge zinaagiza hivyo,” alisema.
Ibara
ya 56 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaongeza utata zaidi katika
suala hilo kutokana na kumzuia mtu yeyote anayeteuliwa kuwa waziri,
kutekeleza majukumu yake kabla ya kula viapo vyote vilivyopo kisheria.
Ibara
hiyo inasema: “Waziri au naibu waziri hatashika madaraka yake ila mpaka
awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine
chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa
mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.”
Mara baada ya kuapishwa Desemba 12, Dk Mahiga alielekea moja kwa moja ofisi za wizara yake kuanza rasmi kazi.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Kafulila amvaa Muhongo
Wakati
huohuo, aliyekuwa mbunge Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila
amesema uteuzi wa Profesa Muhongo umedhihirisha kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano haina nia ya dhati ya kupambana na ufisadi.
“Rais
Magufuli alisema Serikali yake ni ya kutumbua majipu, lakini ni jambo
la kushangaza kuona anaingiza mengine kwenye baraza lake, haeleweki,”
alisema Kafulila alipozungumza na Mwananchi jana kuhusu uteuzi huo.
Kafulila,
ambaye alikuwa kinara wa sakata hilo, alisema Profesa Muhongo ambaye
alikuwa Waziri wa Madini na Nishati wakati fedha hizo zikichotwa,
aliisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
“Nimeshangaa
kuona mtu kama Profesa Muhongo aliyevunja Sheria ya Fedha ya mwaka
2012, Kifungu cha 29 na kusabisha hasara kubwa ameteuliwa kuwa waziri,
tena wa wizara ile ile,” alisema.
Alisema
asilimia 70 ya Sakata la Escrow bado haijaisha. Alidai kuwa Benki ya
Stanbic ambayo ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa
kutoka akaunti hiyo bado mambo hayajamalizika, hata maazimio
yaliyofikiwa na Bunge la 10 Novemba mwaka jana kuhusu sakata hilo bado
hayajatekelezwa yote.
Moja
ya maazimio hayo ni mamlaka husika kutengua uteuzi wa mawaziri
walioguswa na sakata hilo, akiwamo Profesa Muhongo ambaye alitangaza
kujiuzulu mapema mwaka jana.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililla alisema baada ya Bunge la 10 kuvunjwa, shughuli zote za Bunge hilo zilikoma.
“Kama
kuna hoja yoyote ya kuibua hoja za Bunge lililopita, zinatakiwa zianze
upya kwa kufuata taratibu wa Bunge jipya la 11,” alisema Dk Kashililla.
Hata
hivyo, Ikulu ilitangaza Mei mwaka jana kuwa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma imebaini kuwa Profesa Muungo hakufanya vitendo vyovyote
vya ukiukwaji wa maadili katika sakata hilo.
Maoni
Chapisha Maoni