Chadema Wamtaka Rais Magufuli Amfuate Lowassa Ili Amshauri Kuhusu Sukari
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Rais John
Magufuli kuweka siasa kando na kuomba ushauri kwa waziri mkuu wa zamani,
Edward Lowassa ili kutatua tatizo la kuadimika kwa sukari.
Kauli hiyo ilitolewa na naibu katibu mkuu wa Chadema, Salim Mwalimu
juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Moto wilayani
Monduli Mkoa wa Arusha ambako Lowassa alizungumza na wananchi
kuwashukuru kwa kumpigia kura na akatangaza mpango wa kuzunguka nchi
nzima kwa lengo hilo.
Tangu Rais atangaze kudhibiti uagizaji sukari kutoka nje na baadaye
Bodi ya Sukari kutangaza bei elekezi, bidhaa hiyo muhimu imepanda bei
kutoka Sh1,800 hadi kufikia Sh5,000 kwa kilo na kwa sasa imeadimika
madukani, wakati Serikali ikisaka wafanyabiashara inaowatuhumu kuwa
wameificha kwenye maghala kwa lengo la kuihujumu.
Akizungumza kabla ya kumruhusu Lowassa kuongea na wananchi hao,
Mwalimu alisema inaonekana tatizo la sukari linaelekea kuishinda
Serikali na hivyo inahitaji msaada wa ushauri.
“Tatizo la sukari kalianzisha yeye mwenyewe Magufuli na sasa anashindwa kulitatua,” alisema Mwalimu na kuongeza:
“Mtu pekee atakayemsaidia ni Lowassa. Huyu alijipanga na alijiandaa kuongoza nchi.”
Mwalimu alisema Lowassa amevumilia mengi kwa kuwa amenyanyaswa, ameonewa na kusimangwa lakini hakujibu.
“Amepitia kipimo cha mwisho cha utu, ni cha mwisho. Walimuonea
mchana kweupe akavumilia. Walimsimanga mchana kweupe mpaka watoto wadogo
walikuwa wakimuona Lowassa kama vile saizi yao, akavumilia,” alisema Mwalimu.
“Ninajua vijana waliumia, mzee. Lakini leo warudi nyuma
wafikirie maisha yao. Ni nani angetoka nyumbani kwa kauli moja ya
Lowassa, kumshika mtoto wake mkono kumpeleka shule kama Lowassa
angeangalia ushetani na kumuacha Mungu,” alisema akirejea kauli ya
Lowassa kuwa alikuwa akipigiwa simu na watu kumtaka atoe kauli baada ya
matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana kutangazwa, lakini akaawaambia
watulie.
Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema baada ya
kuenguliwa CCM, alishika nafasi ya pili kwenye mbio hizo akipata kura
milioni 6.07 idadi ambayo ni rekodi kwa mgombea wa upinzani tangu siasa
za ushindani zirejeshwe mwaka 1992. Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata
kura milioni 8.8.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Lowassa aliwataka wananchi
kuendelea kutulia, akisema mwaka 2020 hauko mbali na Chadema inaendelea
kujipanga upya ili kuhakikisha inashika dola na kuondoa kero zao.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa
Chadema kutoka makao makuu, mkoa pamoja na makada waliojiunga wakitokea
CCM wa wilaya ya Monduli, Lowassa alisema wafuasi wa ukawa wajiandae kwa
mikutano hiyo.
Huku akishangiliwa na wananchi hao waliokuwa wakimkatisha kwa
kelele za shangwe, Lowassa alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake
wamejipanga kufanya ziara ya kuijenga Chadema nchi nzima.
“Nina hakika tumewashika pabaya CCM na tumewaumiza sana. Sasa
kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tutazunguka nchi nzima tunataka
kuiweka Chadema kwenye chama cha siasa na si uanaharakati,” alisema.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba 25 mwaka jana,
Lowassa aliwashukuru wananchi kwa kumpa kura nyingi akisema hata
walioiba kura zake wanajua na dunia inajua kuwa alishinda.
“Niliamua kukaa kimya kwani najua ningesema jambo moja nchi yetu
ingeangamia. Na vijana kila kona ya nchi walikuwa wakinipigia simu
wakidai wanasubiri neno kutoka kwangu,” alisema.
“Sikufurahishwa na kwenda Ikulu kwa mikono iliyojaa damu. Kuna
siku nitakwenda Ikulu kwa mikono safi ya Watanzania, nina hakika na
rafiki zetu wanajua kabisa kwamba hawakushinda.”
Maoni
Chapisha Maoni