JK Afanya ‘Ukauzu’ Ughaibuni
Mkutano huo ulioanza jana mjini New York, unajadili masuala mbalimbali ikiwemo vita dhidi ya ugaidi pamoja na utolewaji wa misaada zaidi kwa wakimbizi.
Mkanda wa video uliopatikana leo, umemuonyesha Dk. Kikwete akitoka katika eneo la mkutano huku wandishi wa habari wakijaribu kumuhoji lakini akikataa na kuendelea kutembea, akiondoka katika eneo hilo.
Baada ya Dk. Kikwete kukataa kuhojiwa alionekana akiwatupia maneno waandishi hao. Hata hivyo maneno hayo hayakuweza kunaswa na vinasa sauti vya wandishi hao huku msaidizi wake akiwazuia waandishi hao ili wasiendelee kumsogelea.
Haikujulikana mara moja, kwanini Dk. Kikwete alikataa kuzungumza na wandishi wa habari katika eneo la nje ya mkutano huo, ikizingatiwa kwamba katika siku za nyuma amekuwa ‘rafiki’ kwa waandishi.
Dk. Kikwete amehudhuria mkutano huo akiwa ni Balozi wa heshima wa chanjo duniani na Mwenyekiti mwenza wa jopo la watu mashuhuri duniani lenye jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa UN juu ya uboreshaji wa malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals).
Si Dk. Kikwete pekee ‘aliyewachomolea’ waandishi wa habari, isipokuwa hata Christine Lagarde, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la fedha ya kimataifa (IMF), naye hakuwa tayari kuzungumza na wanahabari baada ya kutoka katika mkutano huo.
Mkutano huo wa 71 wa UN umeendelea tena leo ambapo Rais Barrack Obama wa Marekani, amehutubia akizungumzia suala la kuongeza misaada kwa wakimbizi ikiwemo utolewaji wa elimu kwa wakimbizi.
Mwanahalisi online
Maoni
Chapisha Maoni