Wanafunzi 7,000 Watimuliwa UDOM
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimewasimamisha masomo zaidi ya
wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya
stashahada na kuwataka waondoke chuoni hapo mara moja.
Jana, lilitolewa tangazo chuoni hapo likiwataka wanafunzi hao
kuondoka kati ya jana hadi leo saa 12 jioni. Tangazo hilo lilieleza kuwa
kutokana na matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo,
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi imeamua wanafunzi hao kurejea majumbani na wataelezwa mustakabali
wao “mapema iwezekanavyo”.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alipotakiwa
kufafanua suala hilo, alisema kwa ufupi kuwa suala hilo lipo lakini
akaelekeza apigiwe simu Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Beatrice Baltazal
kwa maelezo zaidi.
Baltazal alipotafutwa alisema kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la Serikali na wametakiwa kulitekeleza.
Kuhusu lini na nini hatima ya wanafunzi hao, alisema bado hawajui hadi hapo watakapoelekezwa vinginevyo.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kwa wanafunzi hao juu ya namna
walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao kwa ghafla na kutakiwa
kuondoka.
Kozi ya stashahada ya ualimu wa sayansi, ilianzishwa maalumu kwa
agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuziba pengo la walimu wa
sayansi na ilikuwa inatolewa UDOM pekee.
Waliokuwa na sifa za kujiunga na kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao waliokuwa wamekopeshwa na Serikali wamesimamishwa
siku mbili baada ya wenzao zaidi ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph
kusimamishwa baada ya kubainika hawakuwa na sifa za kudahiliwa.
Facebook Comments
Maoni
Chapisha Maoni