PENZI KWA FLORA ,NAMSHANGAA SANA MBASHA


Mwimbaji wa muziki wa Injili nchini, Emmanuel Mbasha. MWIMBAJI wa muziki wa Injili nchini, Emmanuel Mbasha ameshinda kesi yake ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili, aliyotuhumiwa kumfanyia kitendo hicho msichana aliyekuwa akiwasaidia kazi za ndani ya nyumba yake na aliyekuwa mkewe, Flora Mbasha.Emmanuel Mbasha alidaiwa kufanya kitendo hicho mara mbili kwa msichana huyo, kitu ambacho ni kinyume cha sheria za nchi.
 
Aliyekuwa mke wa Emmanuel Mbasha, Flora Mbasha. Hata hivyo, baada ya takriban mwaka mmoja na ushee, wa kusikiliza pande mbili, Jamhuri iliyomshtaki na kuwasikiliza mashahidi, hatimaye, mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa kijana huyo hana hatia!
Kwa kuwa mahakama ndicho chombo kinachotafsiri sheria, ni vyema nikimpongeza Mbasha kwa matokeo hayo, kwani vinginevyo alikuwa anakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka 30 jela. Kwa umri wake, kama ingethibitika, bila shaka tungemsahau, maana muda huo ni mrefu, ukizingatia kosa lake ni miongoni mwa makosa ambayo hayana msamaha!
Emmanuel Mbasha na aliyekuwa mkewe, Flora Mbasha.Kwa tunaofahamu kidogo mkasa wa kesi hiyo, ni matokeo ya mgogoro wa ndoa yake na mkewe, Flora Mbasha. Ukitazama vizuri maudhui ya shauri hilo, ni vigumu kumtoa mwanamke huyo ambaye pia ni mwimbaji wa Injili kuwa nyuma ya pazia.
Hii inatokana na mambo kadhaa, lakini kubwa zaidi ni kesi hiyo kufunguliwa wakati mgogoro wa kifamilia ukiwa umepamba moto na kibaya zaidi, mkewe kukubali kuwa miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka. Kesi hii ilisikilizwa chemba, hivyo ni vigumu kujua alisema nini, lakini hisia zinakusukuma kuamini kuwa ushahidi wake ulikuwa wa kumkandamiza mumewe!
Nimelazimika kuandika makala haya baada ya kusikia sehemu ya mahojiano ya Mbasha akiwa mahakamani kabla ya kupanda kortini na mwandishi wa gazeti hili, Brighton Masalu. Alimnukuu akisema kuwa licha ya yote yaliyotokea, bado anampenda sana mkewe!
Kwa walioishi na wanaoishi katika ndoa, wanajua. Kuna mambo mengi yanatokea baina ya wanandoa ambayo wakati mwingine yanapotoka nje, yanawaacha watu midomo wazi. Kuna watu wana miaka kadhaa hawasemeshani japo wanaishi nyumba moja, ingawa nje, wanafahamika kuwa mke na mume!
Kinachosababisha yote haya ni uvumilivu wa kila mmoja. Huamua kubaki kimya au liwalo na liwe, lakini anaendelea kuwa na mwenzi wake. Wanaokosa uvumilivu, ndiyo wale tunaosikia wameuana, wamemwagiana tindikali au kupeana ulemavu mwingine wowote.
Lakini kuna mambo ambayo mwenzi mmoja hawezi kumfanyia mwenzake hadharani na jamii ikaona kuwa ni sawa. Kushadadia mume kufungwa katika kesi mbaya kama ya ubakaji, ni miongoni mwa mambo hayo.
Mwanamke anayekupenda, ambaye nawe wapaswa kumlipa upendo, hawezi kuwa shahidi kizimbani dhidi yako katika shauri lenye adhabu kali kama ubakaji. Mtu anayeweza kuthubutu kufanya hivi, ni mwenye moyo wa kuweza kufanya kitu kingine chochote kibaya.
Sisemi Mbasha alipe kisasi, lakini kama mwanaume, nimejisikia vibaya kusikia moyo wake bado unampenda mtu aliyetaka kusababisha afungwe kifungo kirefu. Labda ameitoa kistaarabu kuionesha jamii jinsi alivyo hana kinyongo, jambo ambalo ni zuri, lakini ni vyema akaamini kuwa huyo si mtu salama kwake.
Wanandoa, hasa wenye watoto, wana ukomo wa tofauti zao. Katika hatua ambayo mmoja anaweza kuangamia, moyo wa ajabu hujitokeza na wawili hao huungana na kuwa kitu kimoja.
Siamini kama Mbasha ni miongoni mwa wanaume ambao wapo tayari kufa ili mradi kutetea penzi. Endapo yupo hivi, ningemshauri kujitathmini upya, kwa maana kuna maisha nje ya Flora. Watu tumeumbwa kusamehe, lakini tunakatazwa kusahau.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Nani aligharamia ukarabati wa kifahari wa ofisi ya Mkuu wa mkoa

Abu Bakr al-Baghdadi: Nguo ya ndani ya kiongozi wa IS 'iliibiwa' kufanya uchunguzi wa DNA