Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kulakiwa na Donald Trump Marekani
Rais wa Nigeria
Muhammadu Buhari atakuwa kiongozi wa kwanza wa taifa la kutoka bara
Afrika kulakiwa na Rais wa Marekani Donald Trump White House
atakapokutana na kiongozi huo kwa mashauriano rasmi mjini Washington
baadaye leo.
Marais wengine wa Afrika wamewahi kukutana na Bw
Trump akiwa rais, wakiwemo Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa
Kenya, lakini nje ya Marekani.Rais Kenyatta alikutana na Trump pambizoni mwa mkutano wa G7 nchini Italia mwezi Mei mwaka jana, naye Rais Kagame akakutana na kiongozi huyo wa Marekani Januari mwaka huu mjini Davos, Uswizi pambizoni mwa mkutano mkuu kuhusu uchumi wa dunia.
Septemba mwaka jana, Rais wa Uganda Yoweri Museveni pia alikutana na kupigwa picha na Rais Trump kwenye dhifa iliyoandaliwa wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York. Hakukuwa na mazungumzo yoyote hata hivyo na haikuwa ziara ya kikazi kwa Bw Museveni.
Wawili hao wanatarajiwa kujadiliana kuhusu masuala ya kiuchumi na kiusalama watakapokutana leo.
Lakini wengi watafuatilia kwa karibu mazungumzo hayo hasa baada ya Bw Trump kushutumiwa vikali kutokana na kuyaeleza mataifa ya Afrika kama ''machafu" au ya "mabwege" mapema mwaka huu.
Bw Trump alijitetea na kusema kwamba hakuwa anayabagua mataifa ya Afrika.
Trump na Buhari watazungumzia nini?
Mwandishi wa BBC kutoka Nigeria Mayeni Jones anasema viongozi hao wawili bila shaka watataka kusahau kashfa hiyo na kuangazia mambo ya muhimu zaidi kuhusu uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Nyumbani, Rais Buhari anakabiliwa na changamoot kadha za kiusalama, ikiwa ni pamoja na maasi ya wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na ukosefu wa usalama katika ukanda wa kati wa taifa hilo.
Kwa hivyo, vita dhidi ya ugaidi bila shaka vitapewa kipaumbe na wawili hao, mwandishi wetu anasema.
Marekani imetuma ndege 12 za kivita za kusaidia kukabiliana na waasi wa Boko Haram ambazo ni za thamani ya jumla ya Boko Haram.
- Botswana yamshutumu Trump kwa kutusi nchi za Afrika
- Mataifa ya Afrika yamtaka Trump kuomba msamaha
- Rais Museveni ammwagia sifa Trump
Bw Buhari, ambaye majuzi alitangaza kwamba atawania tena urais mwaka 2019, pia anatarajiwa kusisitiza kujitolea kwake kuendeleza utawala wa kidemokrasia. Serikali yake imeshutumiwa kwa kuendeleza ufisadi na utawala mbaya nchini Nigeria.
Baada ya mazungumzo hayo, Bw Buhari anatarajiwa kukutana na wafanyabiashara wanaoangazia kilimo.
Maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Nigeria pia watafanya mazungumzo na maafisa wakuu wa kampuni kubwa kubwa za uchukuzi Marekani kuhusu miradi kadha ya miundo mbinu.
Maoni
Chapisha Maoni