Kamati ya Bunge Yakataa faini ya 500,000/- Kwa Kila Kosa Barabarani
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa mbele ya kamati hiyo mjini Dodoma jana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Baada ya kuyakataa mapendekezo hayo, kamati hiyo imetoa muda wa siku mbili kwa Sumatra kuhakikisha inawasilisha mbele ya kamati hiyo mapendekezo yanayokubalika.
Sumatra inapendekeza kuongeza kiwango cha adhabu ya faini kutoka kati ya Sh 10,000 na Sh 50,000 hadi Sh 200,000 na 500,000 kwa watoa huduma za uchukuzi, watakaokiuka masharti ya leseni zao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa alisema mapendekezo hayo, yatazidi kuwaongezea mzigo Watanzania badala ya kuwasaidia.
Alisema kiwango hicho cha faini kubwa, kamwe hakitazuia tatizo la ajali za barabarani, zaidi ya kuongeza ukubwa wa tatizo la rushwa.
“Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwasaidia wananchi, lakini mapendekezo haya yatazidi kuwaongezea mzigo kwa sababu kiwango cha faini hizi kama kitapitishwa, watoa huduma za uchukuzi watahamishia hasara yao kwa wananchi,” alisisitiza.
Aliitaka mamlaka hiyo, kwenda kuyafanyia kazi tena mapendekezo hayo kwa kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwasilisha viwango vya faini vinavyokubalika.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Mhagama ambaye pia ni mbunge wa Madaba, alisema mapendekezo hayo hayana nyongeza yoyote, itakayoisaidia serikali katika kudhibiti tatizo la ajali barabarani.
“Kwa sasa serikali imeweka nguvu zake katika kupunguza ajali za barabarani, lakini kiwango cha faini hizi hakina uhusiano wowote na jitihada hizi zaidi ya kuiongezea Sumatra mapato na kuwapa mzigo walipa kodi,” alisema.
Akiwasilisha mapendekezo ya mamlaka hiyo mbele ya Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, yamelenga kuiboresha zaidi sheria hiyo ya leseni za uchukuzi.
Alisema marekebisho hayo, pia yatasaidia mamlaka hizo kuendana na mahitaji ya sasa hasa katika eneo la adhabu ya faini, hali itakayopunguza kiwango kikubwa cha kukiukwa kwa masharti ya leseni
Maoni
Chapisha Maoni